Michezo

Southampton waizima Norwich

June 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABAO matatu ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Southampton uwanjani Carrow Road yalididimiza kabisa matumaini ya Norwich City kusalia kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu huu.

Danny Ings aliwafungulia Southampton ukurasa wa mabao kunako dakika ya 49 kabla ya Stuart Armstrong na Nathan Redmond kupachika mengine wavuni kunako dakika za 54 na 79 mtawalia.

Norwich kwa sasa wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama 21 huku pengo la pointi 16 likitamalaki kati yao na Southampton watakaowaalika Arsenal ugani St Mary’s mnamo Juni 25. Norwich watakuwa wenyeji wa Everton mnamo Juni 24 kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Arsenal, Chelsea na Manchester City kwa usanjari huo.

Wakirejea ugani kwa mara ya kwanza baada ya kukosa kunogesha mechi yoyote kwa kipindi cha siku 104, Norwich ambao kwa sasa wana jumla ya mechi nane pekee ili kuponea msimu huu, walionekana walegevu katika takriban kila idara.

Ingawa hivyo, kinachofisha zaidi matumaini yao finyu ya kusalia ligini muhula ujao ni rekodi ambayo imekuwa ikishuhudia klabu zote zinazojizolea chini ya alama 25 kufikia sasa (mechi 30) katika kampeni za kipute hicho zikiteremka ngazi.

Ushindi kwa Southampton uliwapaisha hadi nafasi ya 13 kwa alama 37, tano pekee nyuma ya Tottenham waliolazimishiwa sare ya 1-1 na Manchester United.

Kabla ya mechi, kocha Daniel Farke wa Norwich alikuwa ameshikilia kwamba kikosi chake kinahitaji kusajili ushindi mara tano pekee kutokana na mechi tisa zilizosalia ili kujipa uhakika wa kunogesha kivumbi cha EPL kwa mara nyingine muhula ujao.

Kipute cha EPL kilipoanza rasmi mnamo Agosti 2019, Ings alikuwa katika fomu nzuri zaidi, akifaulu kuwafungia Southampton jumla ya mabao 10 kutokana na mechi 15 za kwanza baada ya kufanikisha uhamisho wake wa Sh2.8 bilioni kutoka Liverpool.

Hata hivyo, kisu cha makali yake kilionekana kusenea mwishoni mwa Januari 2020 baada ya kupachika wavuni bao moja pekee kutokana na mechi saba kabla ya soka ya Uingereza kusimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona mnamo Machi 13, 2020.