Southampton yaipokeza Liverpool kichapo cha 1-0

Southampton yaipokeza Liverpool kichapo cha 1-0

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Liverpool kuhifadhi taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu yaliyumbishwa Jumatatu usiku baada ya Southampton kuwapokeza kichapo cha 1-0 uwanjani St Mary’s.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Southampton lilipachikwa wavuni na Danny Ings ambaye ni mchezaji wa zamani wa Liverpool. Bao hilo lililojazwa wavuni katika dakika ya pili, lilitokana na frikiki ya James Ward-Prowse aliyemtatiza sana kipa Alisson Becker wa Liverpool katika kipindi cha pili.

Japo Liverpool wanasalia kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 33, masogora hao wa kocha Jurgen Klopp wamejizolea alama mbili pekee kutokana na mechi tatu zilizopita. Hofu zaidi kwa Liverpool ni kwamba wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko nambari mbili Manchester United ambao pia wana alama 33.

Leicester City waliotawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16, wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 32, tatu pekee mbele ya Tottenham Hotspur, Manchester City, Southampton na Everton.

Liverpool kwa sasa wapo katika hatari ya kupitwa na vikosi hivi vyote iwapo watajikwaa katika mechi yao ijayo dhidi ya Man-United mnamo Januari 17 ugani Anfield.

Baada ya kuchuana na Man-United, Liverpool wameratibiwa kucheza dhidi ya Burnley, Tottenham, West Ham United, Brighton, Man-City na Leicester kwa usanjari huo katika EPL.

Ushindi uliosajiliwa na Southampton dhidi ya Liverpool ulikuwa wa kwanza kwa vijana hao wa kocha Ralph Hassenhuttl kutokana na mechi tano zilizopita za EPL.

You can share this post!

Wamiliki wa shule zilizolemewa na makali ya Covid-19...

Muungano wa wanasoka wa Uruguay wataka FA ibatilishe adhabu...