Michezo

Southampton yapanda ngazi kushiriki EPL baada ya kupepeta Leeds United

May 26th, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SOUTHAMPTON wamejiunga tena na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kunyakua tiketi ya mwisho kutoka Ligi ya Daraja la Pili kwa kulipua Leeds 1-0 katika fainali ugani Wembley jijini London, Jumapili.

Saints, ambao walishushwa ngazi kutoka EPL mwisho wa msimu 2022-2023, walipachika goli la kuzamisha Leeds kupitia kwa Adam Armstrong dakika ya 24 baada ya kukamilisha pasi safi kutoka kwa kiungo wa kati William Smallbone.

Southampton waliingia fainali hiyo na motisha ya kupepeta Leeds 3-1 nyumbani mnamo Septemba 30, 2023 na 2-1 ugenini hapo Mei 4 katika msimu wa kawaida.

Leeds sasa wamefika fainali ya Daraja la Pili mara nne; 1986-1987, 2005-2006, 2007-2008 na 2023-2024 bila ya kuzishinda zote.

Vijana wa kocha Russell Martin wanaungana na Leicester na Ipswich Town katika kupandishwa daraja.

Leicester na Ipswich walikamilisha msimu wa kawaida katika nafasi mbili za kwanza ambazo huandamana na tiketi ya moja kwa moja kushiriki EPL.

Leeds, Southampton, West Brom na Norwich walimaliza msimu wa kawaida katika nafasi ya tatu, nne, tano na sita na hivyo wakaingia katika mashindano ya muondoano kujaza nafasi ya mwisho.

Leeds walichapa Norwich 4-0 nao Southampton wakalima West Brom 3-1 katika nusu-fainali.

Leicester, Ipswich na Southampton wamejaza nafasi za Luton Town, Burnley na Sheffield United walioshushwa ngazi baada ya kukamata nafasi tatu za mwisho kwenye EPL msimu 2023-2024.