Michezo

Southgate akiri kukamwa kijasho vilivyo na Kosovo

September 12th, 2019 2 min read

Na LONDON, Uingereza

KOCHA Gareth Southgate wa timu ya Uingereza amekisifu kikosi chake baada ya ushindi wa manbao 4-3 dhidi ya Kosovo, lakini akakiri kwamba timu yake ilifanya makosa ya kujitakia.

Baada ya Kosovo kutangulia kujipatia bao dakika ya kwanza kupitia kwa Valon Berisha, wenyeji walifunga kupitia kwa Raheen Sterling, Harry Kane na bao la kujifunga kabla ya kinda Jodan Sancho kupachika mawili.

Lakini kutokana na makosa katika eneo la hatari, wageni walijipatia mabao mawili kupitia kwa Berisha na Vedat Muriqi kabla ya Kane kupoteza mkwaju wa penalti.

“Tulishinda, lakini upinzani ulikuwa mkali hadi dakika ya mwisho,” Southgate alisema kupitia kwa kituo cha ITV baada ya ushindi wao kwenye mechi hiyo iliyochezewa St Mary’s, Southapmton.

“Tulifungwa mabao kutokana na makosa madogo madogo, lakini nafurahia jinsi tulivyojitahidi na kupata ushindi. Itabidi tujirekebishe kutokana na makosa tuliyofanya.”

Uingereza inaongoza Kundi A kutokana na ushindi mara nne baada ya kujibwaga uwanjani mara nne, tofauti ya pointi tatu mbele ya Jamhuri ya Czech ambao wamefunga mabao 19.

Makosa ya beki Michael Keane yalimwezesha Berisha kuifungia Kosovo bao la mapema na kuongeza mengine mawili, moja likipatikana kutokana na penalti iliyopeanwa baada ya beki Harry Maguire kumchezea ngware mshambuliaji wa Kosovo katika eneo la hatari.

“Sielewi makosa yetu yalitokana na shinikizo ama kuchanganyikiwa, lakini ni suala tutakalotilia mkazo ili tujirekebishe kabla ya mechi ijayo,” alisema mlinzi huyo wa zamani wa klabu ya Middlesbrough, Aston Villa, Crystal Palace na Watford.

“Lakini kilichonifurahisha ni wachezaji kucheza kwa bidii na kuibuka washindi dhidi ya timu limbukeni ambayo ilishangaza wengi uwanjani,” alisema.

“Kwa hakika, walitutatiza, hata kuingia kwa akina Mason Mount mechi ikielekea kumalizika hakukubadilisha mambo. Hata hivyo, tumejifunza kutokana na mechi nzima,” aliongeza.

‘Rekodi si kitu’

Kosovo walifika Southampton wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi 15, baada ya awali kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Czech ambao sasa wamesonga hadi nafasi ya pili baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Montenegro.

Southgate amesifu mchezo wa sasa cha Sterling ambaye mara kwa mara alikuwa mwiba katika safu ya ulinzi ya wapinzani.

Lakini aliiponza safu yake ya ulinzi ikiongozwa na Maguire kwa kufanya makosa kadhaa madogo madogo.

Kwa upande wake, kocha Bernard Challandes wa Kosovo alisema watajirekebisha na kurejea kwa makali zaidi katika mechi zitakazofuata.

Kufikia sasa, Uingereza imefunga mabao 14 nyumbani katika mechi zao tatu za mchujo wa kufuzu kwa Euro 2020, huku Kosovo ikiwa timu ya kwanza kufunga mabao matatu ugenini dhidi ya Uingereza tangu Croatia ifanye hivyo mnamo 2007.