Michezo

Soy United iilivyojikaza kuingia Supa Ligi

November 14th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

SOY United imepandishwa ngazi kushiriki kipute cha Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) muhula huu baada ya kulaza Mulis Children Family (MCF) FC mabao 10-09 kupitia mipigo ya matuta katika Uwanja wa Utalii, Nairobi. Wanadimba hao waligeukia kuamua mshindi kupitia matuta walipoagana sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida.

Soy United ya kocha, Samwel Twago imejiunga na timu zingine mbili zilizojikatia tiketi ya kushiriki ngarambe hiyo kutoka Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza.

MULONDWA

MCF FC iliyopigiwa upatu kutwaa nafasi hiyo chini ya kocha, Ishmael Mbithi ilitangulia kufunga bao hilo dakika ya 65 kupitia Lwanda Mulondwa. Hata hivyo furaha ya wachana nyavu hao ilikatizwa dakika 12 baadaye pale nahodha Timothy Muganda aliposawazishia Soy United.

”Bila shaka haikuwa rahisi lakini tumefanikiwa kubeba tiketi ya kusonga mbele. Mabeki wangu bila kuweka katika kaburi la sahau washambuliji wangu walifanya kazi nzuri licha ya kuonekana kuziwa nguvu na wapinzani wetu,” kocha Twago alisema na kuongeza kuwa sasa wanaanza maandalizi ya kushiriki kipute hicho cha pili pili.

Meneja wa MCF FC, Joseph Kimeu alikubali kushindwa na kusema hawajavunjika moyo bado watajituma kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza wakilenga kujikatia tiketi ya moja kwa moja kupandishwa daraja.

KUZIMA

”Napongeza wachezaji wangu kwa kunyamazisha wapinzani wetu na kunasa tiketi ya kusonga mbele,” patroni wa Soy United, Edwin Ayiro Chahilu alisema na kuwataka kutolaza damu dimbani kwenye mechi za soka za kipute cha BNSL msimu huu.

Bosi huyo anasema wamepania kushiriki migarazano hiyo chini ya msimu miwili au mitatu kisha kupanda ngazi. ”Katika mpango mzima naomba kila mchezaji atambue dhamani yake na kuwajibika ipasavyo dimbani kwenye kampeni za kuwinda tiketi ya kushiriki mechi za ligi ya haiba kubwa nchini,” Patroni akasema.

SILIBWET

MCF FC na Soy United zilijikatia tiketi ya mchezo huo baada ya kila moja kuibuka ya pili katika jedwali la Kundi A na B mtawalia. Katika Jedwali la Kundi A, Mwatate United iliibuka kidedea kwa kuzoa alama 33 nayo Silibwet FC kwa alama 32 ilibeba ubingwa wa Kundi B. Soy FC inajivunia kushinda mataji kadhaa tangia ianzishwe zaidi ya miaka kumi iliyopita ikiwamo Ayiro Tournament, Mafunga Tournament na Cleophas Malala Cup mwaka 2017. Pia inajivunia kukuza wanasoka kadhaa akiwamo Robert Mudenyi Ayala ambaye husakatia AFC Leopards ya Ligi Kuu nchini.