Habari Mseto

Spika alazimika kushuka chini na kuomba Waislamu msamaha

April 20th, 2024 1 min read

NA WINNIE ONYANDO

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Kennedy Ng’ondi amelazimika kuwaomba msamaha viongozi wa dini la Kiislamu nchini kufuatia video iliyosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikionyesha ‘akimlazimisha’ diwani wa dini ya Kiislamu kumkumbatia.

Akizungumza baada ya kukutana na viongozi wa Kitaifa la Waislamu Nchini (SUPKEM), Bw Ng’ondi alisema kuwa anajuta sana kwa kufanya kitendo kama hicho na kwamba hatawahi kurudia tena.

“Nimekuja hapa leo kuwaomba msamaha ndugu zetu. Najuta sana kwa matendo yangu. Sikujua kuwa ingechukuliwa kwa uzito,” akasema Bw Ng’ondi.

Kando na hayo, alimwomba diwani mteule Fatuma Abdi pamoja na familia yake msamaha.

“Nakuomba unisamehe,” akaongeza Bw Ng’ondi.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Viongozi wa Kiislamu Kitaifa (NAMLEF) Abdullahi Abdi, alisema kuwa ni aibu sana kwa kiongozi anayeheshimiwa kufanya kitendo kama hicho.

Hata hivyo, alisema kwamba wamemsamehe Bw Ng’ondi.

“Tunataka hii iwe funzo kwa viongozi wengine. Hatutarajii kitu kama hiki kufanyika tena,” akasema Sheikh Abdi.

Haya yanajiri baada ya spika huyo kujitetea akisema kwamba video hiyo ilichukuliwa 2022 wakisherehekea siku yake ya kuzaliwa.

“Video hiyo ilichukuliwa 2022. Sherehe hiyo iliandaliwa na madiwani wanawake. Sikuwa na nia mbaya. Kadhalika, ninawaheshimu sana akina dada na hasa wale wa dini la Kiislamu,” akasema Bw Ng’ondi.

Kwenye video hiyo, Bw Ng’ondi alionekana akimlazimisha diwani huyo wa kike kusimama na kumkumbatia mbele ya viongozi wenzake.

Video hiyo ilivutia hisia za watu hasa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii huku wengi wakimshambulia spika huyo kwa kitendo hicho walichokiita unyanyasaji wa kimapenzi.