Habari MsetoSiasa

Spika awashauri magavana kuandaa manaibu kuongoza

August 4th, 2019 2 min read

NA VITALIS KIMUTAI

SPIKA wa Bunge la Seneti, Kenneth Lusaka amewashauri magavana kuwateua manaibu wenye tajriba ya uongozi ili kuendeleza ndoto zao iwapo watalazimika kuondoka afisini kabla ya muhula wao kukamilika.

Matamshi ya Bw Lusaka yanajiri huku Dkt Hillary Barchok akitarajiwa kuapishwa gavana wa Bomet wiki hii kufuatia kifo cha aliyekuwa gavana Dkt Joyce Laboso.

Bw Lusaka alisema baadhi ya magavana waliwateua wagombea wenza wadhaifu ili kuzima ushindani wakati wa utawala wao.

“Hatuwatakii magavana chochote kibaya, lakini kikitokea lazima kuwe na mtu mwenye tajriba au ujuzi wa kusimamia kaunti,” akasema Bw Lusaka ambaye alikuwa gavana wa Bungoma kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Dkt Barchok atakuwa gavana wa tatu wa Bomet, miaka saba tangu mfumo wa ugatuzi uanze na ataapishwa Alhamisi wiki hii katika uwanja wa Bomet, eneo ambalo mtangulizi wake alilishwa kiapo Septemba 22, 2017.

Kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM), Isaac Ruto alikuwa gavana wa kwanza wa Bomet na alishindwa kwenye uchaguzi wa 2017 na marehemu Laboso aliyewania kwa tiketi ya chama cha Jubilee.

Idadi hiyo ni ya pili kwani Nyeri inaongoza kwa kuwa na magavana wanne tangu 2013. Hao ni marehemu Nderitu Gachagua ambaye alirithiwa na naibu wake Samuel Wamathai.

Kwenye uchaguzi wa 2017, Wahome Gakuru alichaguliwa lakini akaaga kwenye ajali ya barabarani miezi mitatu baadaye ndiposa Mutahi Kahiga akachukua usukani.

Kupitia notisi iliyochapishwa katika gazeti la Ijumaa ya wiki jana, Katibu wa kaunti Evalyne Rono, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya muda ya sherehe za kumwapisha gavana mpya alisema kinara mpya atachukua usukani siku tano zijazo.

Dkt Barchok wiki jana aliahidi kuendeleza miradi ya maendeleo ya aliyekuwa mkubwa wake na akatangaza kwamba hakukuwa na pengo lolote kwenye uongozi wa kaunti baada ya kifo cha Dkt Laboso.

Kwa mara nyingi kumeshuhudiwa mizozo katika ya magavana na manaibu wao, ambao wanahisi kupuuzwa.

Kaunti ya Nairobi ingali inahudumu bila naibu gavana baada ya Polycarp Igathe kujiuzulu mwaka uliopita, huku wadhifa wa spika pia ukizozaniwa kufuatia kuondolewa kwa Beatrice Elachi na madiwani mwaka jana.

Katika Kaunti ya Kiambu., Gavana Ferdinand Waititu amekuwa na uhusiano mbaya na naibu wake Dkt James Nyoro.