Spika azamisha Azimio bungeni

Spika azamisha Azimio bungeni

NA CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula jana Alhamisi alilazimika kuahirisha kikao cha Bunge hilo baada ya wabunge wa Azimio kuzua fujo na kuvuruga shughuli zake.

Hii ni baada ya Bw Wetang’ula kuamua kwamba, muungano wa Kenya Kwanza (KKA) ndio mrengo wa walio wengi katika Bunge hilo.

Walinzi wa bunge walikuwa na wakati mgumu kuwadhibiti wabunge hao wa Azimio ambao walijaribu kunyakua rungu la mamlaka ya Bunge (Mace).

Katika patashika hilo, Bw Wetang’ula alilazimika kukatiza mjadala kuhusu hotuba ya Rais ambayo ilikuwa imeratibiwa kuendelea hadi saa mbili za usiku.

“Kufuatia vurugu na vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo vimechochewa na baadhi ya wabunge wa Azimio, nimeahirisha hadi Jumanne, Oktoba 11,” akasema.

Katika uamuzi wake, Spika Wetang’ula alisema KKA iliipiku Azimio kiidadi bungeni baada ya wabunge 14 kuhama Azimo na kujiunga na muungano huo unaoongozwa na Rais William Ruto.

“Kwa hivyo, wabunge hao 14 ni sehemu ya muungano wa Kenya Kwanza kwa mtazamo wangu. Wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza ni 179 na wale wa Azimio ni 157 na hiyo ina maana kuwa, Kenya Kwanza ndio mrengo wa walio wengi,” Bw Wetang’ula akaamua.

Wabunge hao 14 walichaguliwa kwa tiketi za vyama vya United Democratic Movement (UDM), Maendeleo Chap Chap (MCC), Pamoja African Alliance (PAA) na Movement for Development and Growth (MDG).

Bw Wetang’ula alisema wabunge wa vyama hivyo, walimwandikia barua wakisema wamehama Azimio na kujiunga na muungano wa KKA.

“Vile vile, barua ambayo nilipokea jana kutoka kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) inaonyesha vyama hivi vinne vimewasilisha kesi mahakamani vikitaka kuruhusiwa kujiondoa Azimio. Kwa hivyo, siwezi kuwanyima uhuru wao wa kutangamana na kufanya maamuzi ya kisiasa, kulingana na vipengele vya 36 na 38, kwa kuwalazimisha kusalia ndani ya Azimio,” Bw Wetang’ula aliongeza.

Hata hivyo, aliungama kuwa kulingana na nakala ya mkataba uliobuni Azimio, vyama hivyo vinne vingali wanachama wa muungano huo unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga.

“Kulingana na orodha ya vyama kwenye miungoni ya kisiasa, iliyowasilishwa katika afisi yangu na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, muungano wa Azimio una wabunge 171. Kwa upande mwingine, muungano wa Kenya Kwanza una jumla ya wabunge 165,” Bw Wetang’ula akasema.

Kufuatia uamuzi wa Alhamisi, sasa muungano wa KKA utawakilishwa na idadi kubwa ya wanachama katika kamati zenye ushawishi mkubwa katika bunge la kitaifa.

Kamati hizo ni kama vile Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC), Kamati ya Uteuzi, Kamati ya Bajeti na kamati ambazo zitafuatilia utendakazi wa wizara za serikali kuu.

Kamati ya Uteuzi (CoA) ndio itawapiga msasa mawaziri wateule 22 waliopendekezwa na Rais Ruto kuongoza wizara mbalimbali za serikali.

Hii ina maana kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa mawaziri hao kuidhinishwa na kamati hiyo na kamati ya bunge lote.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ikabili ufisadi iwapo inataka ustawi

Wawili ndani miaka 30 kwa kuiba teksi kimabavu

T L