Habari MsetoSiasa

Nilikuwa tu refa, Spika Lusaka ajitetea kuhusu kumng’oa Wetang'ula

April 8th, 2018 1 min read

Na MACHARIA MWANGI

SPIKA wa Seneti Kenneth Lusaka amejitenga na kung’olewa kwa Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula kama Kiongozi wa Wachache, akisema kuwa yeye alikuwa tu refa.

Bw Lusaka alikana kujua kuhusu mpango huo ambao alieleza kuwa uliamuliwa na wanachama wa muungano wa NASA.

“Sikushiriki kung’atuliwa kwake. Mimi nilipokea mawasiliano kutoka kwa upande wa NASA kuhusu uamuzi wa kumuondoa kiongozi huyo wa Ford Kenya kutoka kwa nafasi hiyo bungeni,” alieleza katika mahojiano na Taifa Jumapili, pembezoni mwa mkutano wa siku mbili wa Seneti, katika hoteli ya Sarova Woodlands mjini Nakuru.

Wakati huo huo, Bw Lusaka alilaumu uhusiano mbaya katika bunge lililopita kuchangiwa na mivutano ya kisiasa ya baadhi ya viongozi bungeni na magavana wao.

Alisema kuwa mivutano hiyo sasa haitashuhudiwa tena.

Pia alifichua kuwa Kamati ya Seneti ya Uhasibu wa Umma na Uwekezaji itawahoji magavana 33 kuhusu utumizi wa pesa za umma, na inatarajia kuwa watashirikiana nao kufafanua maswali ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu.

“Katika siku za nyuma kumekuwa na mvutano wa wazi baina ya maseneta wanaolenga kuwania ugavana na magavana wao,” alieleza.

Spika huyo alisimulia masaibu yake kama gavana na kusema kuwa “Sitaki gavana yeyote apitie niliyopitia, hakukuwa na usawa na yalitarajiwa kunichafulia sifa.”

Seneta wa Nakuru Susan Kihika pia alihimiza kuwepo kwa ushirikiano huo na kueleza kuwa mkutano wao uliangazia changamoto zilizoshuhudiwa katika Seneti iliyopita.