Habari za Kaunti

Spika Mwambire asisitiza Mung’aro hajageuza bunge la kaunti kikaragosi

January 16th, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

BUNGE la Kaunti ya Kilifi limetetea msimamo wake wa kushirikiana na Gavana Gideon Maitha Mung’aro, baada ya madai kutolewa kuwa gavana huyo anatumia bunge hilo kisiasa, na wala sio kwa manufaa ya wakazi.

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire amedokeza kuwa bunge hilo halitumiki na gavana huyo kama inavyosemekana na wapinzani wa serikali hiyo bali, linatekeleza wajibu wake kisheria kwa manufaa ya wakazi na wenyeji wa kaunti hiyo.

“Sisi kitu ambacho kina manufaa kwa watu wa Kilifi ni lazima tukipitishe. Vile vile ikiwa kuna shida mahali, ni lazima wajibu wetu viongozi kushirikiana na gavana tutafute suluhu. Lakini wengine wanataka watuone tukipigana ndipo waseme tuko kazini,” alisema Bw Mwambire.

Aliongeza kwamba ujasiri sio kupigana bali ni kuelewana.

Kauli ya Bw Mwambire iliungwa mkono na Mwakilishi wa Wadi ya Shella iliyoko mjini Malindi Bw Twahir Abdulkarim ambaye alisema kuwa, uhusiano mwema kati ya ofisi ya gavana na Bunge la Kaunti ya Kilifi umezalisha matunda mema na maendeleo mashinani.

“Sisi hatuwezi kuwa bunge ambalo lina malumbano na gavana kila wakati. Kwa mfano ikiwa gavana ametuletea mswada ndani ya bunge tupeane ufadhili wa elimu kwa watoto wetu, sisi ni nani tukatae? Ikiwa gavana ameleta mswada ndani ya bunge tupatie akina mama na makundi pesa za Wezesha Fund, sisi ni nani tukatae? Kwa hivyo sisi pale ndani ya bunge letu la Kilifi tunawaambia wale ambao wanasema bunge limekorogeka, sisi tunawaambia hadharani peupe ya kwamba sisi wa ‘ndio sir’ tunafanya hayo ili kuhakikisha watu wa Kilifi wanapata waendeleo,” akasema Bw Abdulkarim.

Baadhi ya wakosoaji wa serikali ya Bw Mung’aro waliibua gumzo katika mitandao ya kijamii ikiwemo makundi ya WhatsApp na Facebook, wakidai kwamba bunge hilo limekosa uhuru wa kuwajibika na badala yake limekuwa likifuata kile ambacho gavana wa kaunti hiyo anasema.