Makala

Spika wa Bunge aliyeanza maisha kama ‘beach boy’

April 23rd, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

“HAIJALISHI utokako. Cha msingi ni ulipo sasa na unakoelekea. Ila usiudharau mwanzo wako. Ndio uliokupandisha hatua moja na nyingine, hadi ukafikia ulipo.”

Hiyo ni kauli ya Spika wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Azhar Ali Mbarak.

Kwenye mahojiano ya pekee na Taifa Dijitali ofisini mwake, Bw Mbarak alifunguka jinsi maisha yake ya awali yalivyokuwa ya taabu.

Alizaliwa katika familia ya tabaka la chini.

Bw Mbarak,41, ni kitinda mimba katika familia ya watoto sita wa Mzee Ali Mbarak na Bi Umi Sadique Abubakar.

Babake alikuwa mchimba mawe ya ujenzi kwenye migodi ya Manda-Maweni iliyoko wadi ya Shela, Kaunti ya Lamu ilhali mamake akiwa mke wa nyumba tu.

Alijiunga na Shule ya Msingi ya Shela kati ya 1991 na 1999 na kuhitimu masomo yake ya darasa la nane (KCPE).

Kutokana na umaskini uliogubika familia yake, hakuweza kusonga mbele kimasomo.

Ikumbukwe miaka hata kabla ya kufanya KCPE, Bw Mbarak alikuwa mara nyingi akilazimika kuharakisha kutoka shuleni na kufika nyumbani jioni.

Alikuwa akibwaga mkoba wake wa vitabu na kisha kuingia ufukweni kutafuta riziki, iwe ni kupitia uvuvi au kuendesha mashua za watalii baharini ilmradi ajipatie mtaji wa kujikimu na wazazi wake.

Punde alipokamilisha masomo ya shule ya msingi mwaka 1991 na kukosa karo ya kujiunga na sekondari, alijitosa mzimamzima kwenye shughuli za matembezi ya watalii ufuoni, almaarufu ‘beach boy.’

Huduma za Bw Mbarak pia zilijumuisha kutumia mashua kuendesha wageni na watalii hao, kazi aliyoifanya kwa takriban miaka minane.

“Nilizaliwa katika familia ya hadhi ya chini. Babangu alifanya kazi za sulubu, ikiwemo kuchimba mawe ili kuikimu familia yetu. Mama hakuwa na ajira ila alitutunza nyumbani. Hali ngumu ya maisha nyumbani ilinisukuma kuingilia kazi za matembezi ya watalii ufuoni nikiwa umri mdogo,” akasema Bw Mbarak.

Ni kupitia kazi hiyo ambapo alipata fursa ya kutangamana, kutagusana na kuingiliana vyema na jamii yake ya Shela, wageni na watalii, iwe ni wa ndani kwa ndani au wale wa kimataifa waliofika eneo hilo.

Mnamo 2007, akiwa umri wa miaka 24 peke, aliafikia kujaribu bahati yake katika ulingo wa siasa, ikizingatiwa kuwa alikuwa tayari kashajijengea jina Shela la Lamu.

Alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha kiti cha diwani wa wadi hiyo ya Shela, wakati huo akiwa ndiye mgombea wa umri mdogo zaidi. Alishinda uchaguzi huo.

Mnamo 2012 kabla ya mfumo wa ugatuzi kuanza, Bw Mbarak alitumia fedha chache alizokuwa amekusanya kujiunga na shule moja ya upili ya kibinafsi mjini Mombasa kama mtahiniwa wa kujisimamia.

Alifaulu kufanya mtihani wake wa kidato cha nne (KCSE) mnamo 2013, hivyo kujipatia cheti.

Mwaka huo huo wa 2013, Bw Mbarak akajitosa tena kwenye kinyang’anyiro cha Mwakilishi wa Wadi (MCA) eneo hilo la Shela kupitia tiketi ya chama cha ODM na kuibuka mshinda tena.

Pia alihifadhi kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Katika Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Mbarak amewahi kuhudumia nyadhifa mbalimbali, ikiwemo ikiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusu masuala ya Makadirio na Bajeti.

Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9,2022 ulipowadia, Bw Mbarak alitetea kiti chake cha udiwani kwa mara nyingine na kushinda kupitia tiketi ya chama cha ODM kilichoko kwenye mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya.

Alijiuzulu wiki chache baadaye kwa minajili ya kupata mwanya wa kuwania kiti cha Spika wa Bunge la Kaunti ya Lamu.

Alishinda uchaguzi huo wa Spika mnamo Septemba 22,2022, kinyang’anyiro kilichoshuhudia upinzani mkali kutoka kwa diwani mteule wa zamani wa bunge hilo la Lamu, Bw Salim Al-Busaidy, almaarufu Giraffe, aliyejizolea kura 8 nyuma ya Bw Mbarak aliyepata kura 10 katika awamu ya kwanza na ya pili ya kipute hicho.

“Sijazaliwa kwa familia tajiri au ya wanasiasa. Kuishi kwangu vyema na watu ndiko kunanifanya kila ninaposimama kuwania wadhfa fulani ninashinda. Kama Spika, niko chonjo kuendelea kuwahudumia watu wa Lamu ipasavyo,” akasema Bw Mbarak.

Anamkumbuka vyema babu yake mzaa mama, Bw Sadique Abubakar kwa malezi mema yaliyosaidia kumnoa, hasa katika masuala ya uongozi.

“Babu yangu alikuwa mtu wa hekima. Hakusoma lakini jamii ya Lamu ilimthamini na kumheshimu pakubwa. Alihudumu kama mzee wa mtaa wa Shela lakini wanasiasa kwa wakati huo niliwashuhudia wakimtafuta babu yangu kuuliza mashauri kuhusu uongozi na busara zake. Ninaamini hulka yangu ya uongozi inatokana na babu yangu,” akasema Bw Mbarak.

Pia alitaja wanasiasa wakongwe wa Lamu, ikiwemo Mbunge wa zamani wa Lamu Mashariki na aliyekuwa Spika wa Lamu, Mohammed Abu Chiaba na Mbunge wa zamani wa Lamu Magharibi na aliyekuwa gavana wa Lamu, Fahim Yasin Twaha, kwa maelekezo yao yaliyomsaidia kutia fora katika safari yake ya siasa.

Kila anapotafakari kuhusu maisha yake ya awali aidha, Bw Mbarak anashikilia kuwa katu hajuti kwamba kwa wakati mmoja aliwahi kuwa ‘beach boy’ kwenye fukwe za Bahari Hindi Lamu.

Anasema ni kupitia kazi yake ya awali ya ‘beach boy’ ambayo ilimnoa, kumtia makali na kumwandaa vilivyo, hivyo kuweza kustahimili au kuyadhibiti kwa weledi mkuu majukumu yoyote mazito yanayomjia mbele yake, ikiwemo wakati huu ambapo anahudumu kama Spika wa Bunge la Kaunti ya Lamu.

Bw Azhar alizaliwa kijiji cha Shela, kisiwani Lamu mnamo Julai 4,1983.

Ana mke na ni baba wa watoto wane, ikiwemo wavulana watatu na msichana mmoja.