Habari

Spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi ajiuzulu

August 11th, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amejiuzulu; akimuachia naibu wake John Kamangu majukumu hadi atakapopatikana spika mpya.

Elachi amesikitika akisema Kenya ingali haijapiga hatua kuinua hadhi ya wanawake hasa katika nyadhifa za uongozi.

Aidha, amemshukuru Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa kumuunga mkono kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Licha ya kwamba ninatoka, ninajua kwamba Nairobi itatia fora kimaendeleo ikizingatiwa iko chini ya Nairobi Metropolitan Services (NMS) na Rais Kenyatta atakuwa na la kujivunia atakapostaafu,” amesema Elachi.

Kiongozi huyo amemtaka Gavana wa Nairobi Mike Sonko awe mwadilifu na “ninaomba Mungu amwelekeze awe mtu muungwana.”

Amesema anatarajia kwamba itatokea siku ambayo ataandika kitabu kuhusu sarakasi za City Hall yaani ‘City Hall Chronicles’.