Habari

Spika wa Tanzania arai wabunge nchini Kenya watumie Kiswahili

November 1st, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa bunge la Tanzania Job Yustino Ndugai amewataka wabunge kutumia Kiswahili katika mijadala yao kwa sababu ndio lugha inayoeleweka na wengi nchini.

Akiongea Alhamisi alipoongoza hafla ya uzinduzi wa nakala za kanuni za bunge zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, Bw Ndugai alisema ni kinaya kwamba wabunge wa Kenya hutumia Kiswahili wanapoendesha kampeni za kuomba kura lakini pindi wanapoingia bungeni, huipa kisogo lugha hii.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa makini kampeni zinazoendelea za uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Kibra. Wawaniaji wote wanatumia Kiswahili kusaka kura namna ambavyo wengi wenu mlikuwa mkifanya kabla ya uchaguzi mkuu uliopita. Hamfai kuwa wanyonge wa kutumia Kiswahili katika shughuli zenu bungeni,” Bw Ndugai akasema katika majengo ya bunge, Nairobi.

Alisema wabunge wa Kenya wanafaa kukienzi Kiswahili kwa sababu ndiyo lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU), kando na kwamba inatumika kwa wingi katika mataifa ya mashariki, kati na mashariki mwa Afrika

 

Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya Justin Muturi (kushoto) akiwa na mwenzake wa Tanzania Job Yustino Ndugai katika majengo ya bunge Oktoba 31, 2019, wakati wa uzinduzi wa Nakala za Kiswahili za Kanuni za Bunge. Picha/ Jeff Angote

Bw Ndugai alisema Kiswahili kinatumika katika shughuli zote za bunge la Tanzania, ingawa wabunge pia hutumia Kiingereza ambayo ni mojawapo ya lugha rasmi katika bunge hilo.

“Kule kwetu shughuli zote za bunge na kamati zake zinaendeshwa kwa Kiswahili. Kwa hivyo, mkija kule mtapata kanuni za bunge letu zimeandikwa kwa Kiswahili, na kila kikao kinaendeshwa kwa lugha hii,” Bw Ndugai akasema.

Hata hivyo, Bw Ndugai aliwapongeza Wakenya kwa kuchangia maendeleo ya Kiswahili kupitia matumizi ya misamiati mipya ambayo wamekumbatia nchini Tanzania.