Habari za Kitaifa

Spika Wisdom Mwamburi wa Taita Taveta afutwa kwa madai ya kuwa na kiburi


SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Taita Taveta, Bw Wisdom Mwamburi, amebanduliwa mamlakani. 

Hoja ya kumwondoa afisini ilipitishwa kwa kauli moja na wawakilishi 27 kati ya 31.

Mwakilishi mmoja alipinga kuondolewa kwake, mmoja alijiondoa, na mmoja hakuwepo wakati wa kikao cha Jumatano kilichokuwa kikiongozwa na kaimu Spika, Anselm Mwadime.

Hoja ya kumwondoa iliyowasilishwa na Diwani Maalum, Bi Rose Shingira, ilimtuhumu Bw Mwamburi kwa utovu wa nidhamu, kupoteza imani ya wajumbe wa bunge hilo, na kutokuwa na uwezo wa kushikilia nafasi hiyo.

Bi Shingira alimtuhumu spika huyo kwa upendeleo, kushindwa kutoa taarifa sahihi, na kushindwa kutekeleza majukumu yake kama mwenyekiti wa bunge.

“Mara nyingi, alijichanganya mwenyewe na kutoa uamuzi usiofaa unaofaidi upande fulani wa wabunge. Hakuwa na uwezo wa kuelewa na kutekeleza kanuni za bunge na sheria za spika, hivyo kuathiri ubora wa mijadala na shughuli za bunge,” alisema.

Bi Shingira alisema kuwa Spika Mwamhuri hakuwa akishughulikia maslahi ya wabunge kwa kutolipa marupurupu yao, jambo ambalo linaonyesha kiburi na kutokuwa na uwezo wa kusimamia shughuli za bunge.

“Kama mwenyekiti wa bodi ya bunge la kaunti, hawezi kudai kutokuwa na habari kuhusu marupurupu ya wawakilishi na wafanyakazi,” alisema.

Mwakilishi huyo alisema kuwa kushindwa kwa spika kuendesha bunge la kaunti kulingana na matarajio ya wabunge kumekwamisha shughuli za asasi hiyo.

Baada ya kuondolewa kwake, mwakilishi wa Wadi ya Mwanda/Mghange, Bw Mwadime, ambaye pia alikuwa naibu spika, alichaguliwa bila kupingwa kushikilia nafasi hiyo kwa muda.

Aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Gavana Andrew Mwadime na wawakilishi wadi ili kutimiza majukumu yao na kuleta mabadiliko katika kaunti hiyo.

“Wajibu wetu wa kwanza ni uwakilishi, kutunga sheria, na kufanya usimamizi wa serikali ya kaunti kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wa kaunti hii. Tuchukue hatua madhubuti kuitikia wito wa kuwahudumia wananchi,” alisema.

Mnamo Jumatano, Bw Mwamburi hakujitokeza mbele ya bunge kujitetea dhidi ya tuhuma hizo, hata hivyo duru za kuaminika zilisema kuwa alikuwa anapanga kuelekea mahakamani kuzuia kuondolewa kwake.

Mwakilishi wa wadi ya Rong’e, Bi Dorcas Mlughu, alipinga hoja hiyo na kuonekana kuwa pekee aliyekuwa kwenye upande wa spika huyo.

Wakati wa uongozi wa Bw Mwamburi, bunge hilo la tatu lilikabiliwa na shutuma za kutodumisha uwazi na uwajibikaji, na utawala mbovu.

Bunge hilo lilishutumiwa kwa ufujaji wa fedha kupitia wawakilishi kwenda safari za nje ya nchi.

Mnamo Novemba 2022, wabunge 21 walisafiri kisiwani Zanzibar, safari ambayo iligharimu takriban Sh7 milioni.

Mnamo Februari mwaka huu, naibu spika Bw Mwadime alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi kufuatia safari hiyo ya Zanzibar lakini hivi karibuni alifutiwa mashtaka hayo.

Karani wa bunge hilo Bw Gadiel Maganga ambaye pia alikabiliwa na tuhuma hizo bado hajafikishwa kortini kujibu mashtaka hayo.