Dondoo

Sponsa afukuza demu kwa kukojoa kitandani

September 10th, 2019 1 min read

NA CORNELIUS MUTISYA

GREEN PARK,  ATHIRIVER

DEMU mmoja alifukuzwa na sponsa wake mtaani hapa kwa sababu ya kukojoa kitandani.

Kulingana na mdokezi, demu alijiunga na chuo kimoja jijini na katika pilkapilka zake, alikutana na buda mmoja aliyekuwa mkwasi wa kutajika na wakaanza uhusiano.

“Demu alikuwa na bahati aliponasa buda mmoja sonko. Hata alikuwa akimlipia karo yote ya chuoni na kukidhi mahitaji yake ya kimsingi mpaka wanachuo wenzake wakaanza kumuogopa kwa ufanisi aliokuwa nao,” asema mdokezi.

Twaarifiwa kwamba, usuhuba wa wawili hao uliponoga, buda aliamua kumkodishia nyumba ya kifahari mtaani hapa na hata akamnunulia gari La kumpeleka chuoni. Walikuwa wakiishi pamoja kama mtu na mkewe wa ndoa. Hata wanachuo wenzake walikuwa wamempachika jina la makeke “mke wa sonko”.

Inasemekana kwamba, demu hakuwa mpenda mvinyo. Hata hivyo, buda alimshinikiza aanze kubugia pombe na wakawa wanajivinjari katika kumbi mbalimbali za starehe mjini Mlolongo na hata jijini Nairobi. Walikuwa wakirejea makwao usiku wa manane wakiwa wamelewa chakari.

Hata hivyo, kwa kuwa demu hakuwa amezoea kunywa pombe, alikuwa akikojoa kitandani na hata kumlowesha buda kwa mkojo. Tabia hiyo ilimkera buda sana.

“Buda alikerwa mno na tabia ya demu huyo ya kukojoa kitandani kiholela. Licha ya kumwambia aweke spidi gavana, demu alizidi kukojoa kitandani kila akilewa na kusababisha uhusiano wao kuingia doa,” asema mdaku wetu.

Siku ya tukio, wawili hao walitoka kuburudika katika kilabu moja maarufu mjini Mlolongo na wakarejea nyumbani usiku wa manane. Walipojilaza kitandani, demu aliachilia mfereji kama kawaida na ikamlazimu buda alale sebuleni.

Kulipokucha, buda alimshurutisha demu kufunganya virago vyake na kuondoka.