Habari

SportPesa, Betin zasitisha shughuli Kenya

September 28th, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

KAMPUNI za ubashiri wa matokeo ya michezo za SportPesa na Betin, zimefunga shughuli nchini kwa sababu ya mvutano usiyoisha baina yao na serikali kuhusu ushuru na sheria.

Kupitia ilani kwa wafanyakazi wake, Mkurugenzi wa Betin kwa niaba ya kampuni ya Gamecode, pia alitoa notisi ya kuwafuta kazi wafanyakazi wote akitaja changamoto za kifedha.

“Kutokana na kuzorota kifaida, usimamizi umelazimika kufikiria upya kuhusu mfumo wake wa utendakazi na kuendelea na hatua ya kuwafuta wafanyakazi kwa kuwa hawahitajiki tena,” ilisema sehemu ya memo hiyo.

Kulingana na Betin, juhudi za kutafuta suluhu kati ya Julai na Septemba mwaka huu zimegonga mwamba na kuifanya kuwa vigumu kudumisha wafanyakazi.

Kwa upande wake, SportPesa ilielezea kutamaushwa kwao na uamuzi wa serikali wa kutoza ushuru wa asilimia 20 kwa kila ushindi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, SportPesa ilimshutumu aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich kwa hatua hiyo.

“Hadi wakati ambapo kutozwa ushuru wa kutosha na mazingira mema ya sheria yatakaporejeshwa, SportPesa itasitisha shughuli zake nchini Kenya,” ikasema sehemu ya taarifa.