Habari Mseto

Sportpesa na Betin zatakiwa kuilipa KRA Sh8.5 bilioni

June 18th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) inataka kampuni ya mawasiliano ya simu ya Safaricom kukata kima cha Sh8.59 bilioni, ushuru inayodai kampuni mbili za uchezaji kamari.

Kampuni ya Sportpesa, na ile ya Betin Kenya, zinadaiwa ushuru huo ambao kulingana na KRA hazijalipa.

Meneja wa KRA wa anayehusika katika ukusanyaji wa ushuru Asha Salim, alimwandikia Mkurugenzi Mkuu wa Safaricom Bob Collymore na kusema kampuni hiyo ni ajenti wa kushikilia ushuru kwa niaba ya SportPesa na Betin na mamlaka hiyo inahitaji pesa hizo kulipwa.

KRA inaitaka Safaricom kulipa Sh5.29 bilioni inazodai Gamcode Limited, ambayo inafanya biashara kama Betin na zingine Sh3.29 bilioni kutoka kwa kampuni ya Pevans East Africa, ambayo huendesha biashara kama SportPesa.

Zaidi, KRA iliipa Safaricom akaunti ya Benki Kuu ya Kenya kulipa ushuru huo mara moja.

Kampuni za mawasiliano ya simu kama vile Safaricom na Airtel hutoa jukwaa kwa wateja wa kampuni za uchezaji kamari kuweka pesa kielektroniki ili kucheza, na kutoa baada ya kushinda.

Kwa upande wake, kampuni hizo hujipa mapato kupitia kwa ada ya kutoa au kuweka pesa.

Mgogoro kati ya KRA na kampuni hizo huenda ukaathiri leseni zake za kuhudumu.

Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i tayari ameonya kuwa leseni za kampuni za uchezaji kamari zitasimamishwa katika muda wa wiki mbili zijazo ikiwa hazitathibitisha kuwa huwa zinalipa ushuru kiporo.