Michezo

SportPesa yarejea

November 20th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SEKTA ya kamari imepata mwamko mpya baada Bodi ya Kudhibiti Kamari Nchini (BCLB) kurejesha leseni ya kuhudumu ya kampuni ya kamari ya SportPesa ambayo sasa itahudumu chini ya mwavuli wa kampuni ya Milestone Games Ltd.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa, bodi hiyo pia imetangaza kuwa imefutilia mbali mkutano ambao ingeongoza Novemba 26 kujadili suala hilo.

“Kwa mujibu wa kipengele 4 (1) (b) cha Sheria kuhusu Michezo ya Kamari, ibara ya 131 ya Sheria za Kenya, uamuzi wa kufutiliwa mbali kwa leseni yenu ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021 umesitishwa,” bodi hiyo ikasema kwenye taarifa ambayo nakala yake ilitumiwa SportPesa.

Ikaongeza, “Vile vile barua yetu ya Oktoba 30 na inayotajwa hapa imeondolewa sawa na kufutiliwa kwa mkutano ambao ulipangiwa kufanyika mnamo Novemba 26.”

Hayo yanajiri siku moja baada ya Jaji mmoja kupinga hatua ya kuzimwa kwa matumizi ya jina la kibiashara, SportPesa.

Jaji Paul Nyamweya aliruhusu kampuni ya Milestone Games Ltd kutumia nambari za Safaricom za malipo (Pay Bill Numbers) pamoja na nembo ya SportsPesa.

Uamuzi wa jaji huyo ulitolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na Milestone Games Ltd ikipinga hatua ya bodi ya BCLB kuizuia kutumia nembo ya SportPesa na nambari zake za malipo iliyopewa na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom. BCLB ilitoa uamuzi wake mnamo Oktoba 30, 2020.

Bodi hiyo pia ilizuia Milestone Games Ltd kutumia wavuti www.ke.sportpesa.com, nambari ya kodi 29050, 79079 na nambari za “pay bill”.

Hiyo ndiyo maana kampuni hiyo ilielekea kortini kutaka kubatilisha uamuzi huo wa bodi ya BCLB. Mahakama iliamua kuwa bodi hiyo ilichukua hatua hiyo kinyume cha mamlaka yake.

Kurejeshwa kwa leseni ya SportPesa kando na kufufua ari ya kamari miongoni mwa Wakenya, uraibu ambao una madhara yake, pia ni habari njema kwa sekta ya michezo nchini ambayo ilikuwa ikipata udhamini kutoka kwa kampuni hiyo maarufu ya kamari.