HabariMichezo

Sportpesa yaruhusiwa kerejelea biashara

September 3rd, 2019 1 min read

NA BRIAN OKINDA

[email protected]

KAMPUNI ya Sportpesa imejiunga na baadhi ya kampuni zingine za kamari nchini zilizoruhusiwa kurejelea kutekeleza shughuli zao za bahati nasibu baada ya kuzuiliwa kufanya hivyo kwa muda.

Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini, KRA Jumanne iliidhinisha kurudishwa kwa leseni ya kampuni hiyo baada ya kuzimwa kwa muda wa miezi miwili.

Katika ujumbe uliotumwa kwa vyombo vya habari, kampuni hiyo ilisema kuwa imekuwa ikijadiliana na washikadau, na pia wadhibiti wa ushuru kutoka kwa serikali kuhusu leseni yake, majadiliano ambayo yalinuia kueleza vyema madhumuni na sheria ambazo zinahitajiwa kufuatwa, ikiwemo ile ya kulipa ushuru.

“Tumekuwa na majadiliano ambayo yamenawiri na tuna furaha kuwa shirika la kutoza ushuru nchini limekubali kutupea upya leseni yetu. Tuna imani kuwa majadiliano haya yote yatakamilika hivi karibuni ili tuweze kuendelea na shughli zetu za awali,” ujumbe wa Sportpesa ulisema.

Taarifa hiyo ilizidi kueleza kuwa kampuni hiyo inawashukuru wafanyikazi na mashabiki wake wote, na hivi karibuni, itatoa ujumbe kueleza itakapokua ikirejelea shughli zake.

“Sportpesa inaahidi kujitolea kwake kusaidia jitihada za serikali kutekeleza maendeleo nchini, kwa kuendeleza shugli zake ikizingatia sheria za serikali ikiwemo ile ya kutoa ushuru,” taarifa hiyo ilisema.

Kampuni hiyo ya kamari ilikua miongoni mwa zingine zikiwemo Betin, Betway, Betpawa, Premierbet, Lucky 2U, 1XBet, Mozzartbet, Dafabet, World Sport Bet, Atari Gaming, Palmsbet, Bet Boss, Betyetu, Elitebet, Bungabet, Cysabet, Nestbet, Easybet, Kick Off, Millionaire Sports Bet, Kenya Sports Bet na Eastleighbet, ambazo leseni zao zilifutiliwa mbali na serikali mwezi Julai, kwa shutuma za kutolipa ushuru.

Serikali ilidai kuwa kampuni hizi zilikuwa zinapata faida ya kiasi cha Sh200 bilioni kila mwaka ila yalitoa ushuru wa shilingi Sh4 bilioni tu, mwaka uliopita.

Mkurugenzi mkuu wa Sportpesa, Ronald Karauri, hata hivo alikana madai haya, hasa ile inayohusu kiwango cha ushuru.