Spurs waadhibu Wolves na kujiweka pazuri kufuzu kwa Europa League mnamo 2021-22

Spurs waadhibu Wolves na kujiweka pazuri kufuzu kwa Europa League mnamo 2021-22

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur waliimarisha nafasi yao ya kukamilisha kinyang’anyiro cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu ndani ya orodha ya saba-bora na kufuzu kwa soka ya Europa League msimu ujao wa 2021-22.

Hii ni baada ya masogora hao wa kocha mshikilizi Ryan Mason kuwacharaza Wolves 2-0 mnamo Mei 16, 2021 na kupaa hadi nafasi ya sita kwa alama 59 sawa na West Ham United ya kocha David Moyes. Everton walioduwazwa na Sheffield United kwa kichapo cha 1-0 ugani Goodison Park wanakamata nafasi ya nane kwa alama tatu nyuma ya Spurs na West Ham.

Spurs walianika mapema maazimio yao ya kushinda mechi hiyo baada ya kushuhudia makombora matatu ya mafowadi wao yakigonga mwamba wa lango la Wolves mwanzoni mwa kipindi cha kwanza.

Harry Kane alifungulia Spurs ukurasa wa mabao katika dakika ya 45 kabla ya Pierre-Emile Hojbjerg aliyechangia bao hilo kufungia waajiri wake goli la pili kunako dakika ya 62. Spurs nusura wafunge bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili ila fataki ya fowadi Gareth Bale likapanguliwa na kipa wa Wolves, Rui Patricio.

Romain Saiss, Adama Traore na Fabio Silva walipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo zingewawezesha Wolves kufunga magoli ya kusawazisha na hata kushinda mechi hiyo.

Hata hivyo, kichapo kiliwasaza Wolves wanaonolewa na kocha Nuno Espirito Santo katika nafasi ya 12 kwa pointi 45. Ilivyo, Wolves watakamilisha kampeni za msimu huu katika nafasi ya chini zaidi kuliko jinsi walivyofanya katika kipindi cha misimu miwili iliyopita tangu wapandishwe ngazi kushiriki soka ya EPL mnamo 2018-19.

Tottenham watakuwa wageni wa Aston Villa katika mchuano wao ujao ligini mnamo Mei 19 huku Wolves wakiwaendea Everton ugani Goodison Park.

MATOKEO YA EPL (Mei 16, 2021):

Palace 3-2 Aston Villa

Tottenham 2-0 Wolves

West Brom 1-2 Liverpool

Everton 0-1 Sheffield Utd

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jubilee yapiga kampeni kali za kupangua UDA uchaguzini Rurii

Demu aachwa kwa kukwamilia mzinga