Michezo

Spurs wajinasia beki matata Matt Doherty kutoka Wolves

August 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

TOTTENHAM Hotspur wamemsajili beki Matt Doherty, 28, kutoka Wolves ambao pia wanashiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nyota huyo ambaye amesajiliwa kwa kiasi kisichojulikana cha pesa, ametia saini mkataba wa miaka minne kambini mwa Tottenham.

Hadi alipoagana na Wolves, Doherty alikuwa amechezea kikosi hicho jumla ya michuano 300 tangu ajiunge nacho mnamo 2010 kutoka Bohemians ya Ligi Kuu ya Ireland.

Anakuwa mwanasoka wa tatu kuingia katika sajili rasmi ya kocha Jose Mourinho ambaye pia amejinasia huduma za kipa Joe Hart na kiungo Pierre-Emile Hojbjerg.

“Ni fahari tele kuwa sehemu ya kikosi hiki cha haiba kubwa. Ni tija kwamba nitakuwa nikichezea hapa Tottenham ambao wanajivunia uwanja bora zaidi duniani na kocha mwenye tajriba pana katika ulingo wa soka. Hizi ni baadhi ya sababu zilizofanya maamuzi ya kuagana na Wolves kuwa mepesi,” akasema Doherty.

Doherty alishiriki kila mchuano uliopigwa na Wolves katika soka ya EPL msimu huu wa 2019-20 chini ya kocha Nuno Espirito Santo.

Ushawishi wake ugani ulisaidia kikosi hicho kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya saba jedwalini kwa mara ya pili mfululizo tangu wapandishwe ngazi kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).

Licha ya kutinga robo-fainali za Europa League msimu wa 2019-20, Wolves hawakufuzu kwa soka ya bara Ulaya muhula ujao wa 2020-21 baada ya Arsenal waliomaliza kampeni za EPL katika nafasi ya nane jedwalini kunyanyua ubingwa wa Kombe la FA baada ya kuwalaza Chelsea 2-1 kwenye fainali ya iliyochezewa ugani Wembley, Uingereza.

Kwa upande wao, Tottenham walifuzu kwa Europa League msimu ujao baada ya kukamilisha kampeni zao za EPL katika nafasi ya sita kwa alama 59 sawa na Wolves. Masogora hao wa Mourinho waliorodheshwa mbele ya Wolves kutokana na wingi wa mabao.