Michezo

Spurs wana mtihani dhidi ya RB Leipzig Uefa

February 19th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

TOTTENHAM Hotspur ina mtihani mgumu inapokutana na RB Leipzig ya Ujerumani leo Jumatano usiku jijini hapa katika pambano la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), hatua ya maondoano.

Mtihani wa kocha Jose Mourinho wa Spurs unaonekana mgumu inapozingatiwa kuwa Leipzig kwa sasa inakamata nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Bundesliga kwa alama 45, moja nyuma ya Bayern Munich iliyopepeta vibaya Spurs mwaka jana.

Hata hivyo, ingawa alianza vibaya huduma yake jijini hapa tangu achukue usukani kuinoa Tottenham Hotspur, Mourinho ameanza kufurahia baada ya timu hiyo kutoshindwa katika mechi zake za karibuni.

Sare ya mabao 1-1 na Southampton kisha 0-0 dhidi ya Watford zinajumuishwa kwenye matokeo hayo, lakini Spurs walifanikiwa kushinda Norwich na Southampton katika mechi za marudiano ya Kombe la FA Cup majuzi kabla ya kuangusha Aston Villa kwenye ligi kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa wiki.

Awali, kikosi hicho cha Mourinho kilionyesha ujasiri kwa kuwabwaga vigogo Manchester City kwa 2-0 katika mechi ya ligi kuu.

Katika safari ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), mashabiki walishuhudia vijana hao wakianza kampeni yao kwa sare ya 2-2 na Olympiakos, kabla ya kuraruliwa 7-2 na Bayern Munich.

Hatimaye waliibwaga Red Star Belgrade 5-0 kabla ya kuondoka na ushindi wa 4-0 katika mechi ya marudiano.

Ushindi wa 4-2 dhidi ya Olympiakos ulirejesha matumaini yao, kabla ya kupokea kichapo cha 3-1 kutoka kwa Bayern.

Kwa upande wa RB Leipzig, walianza kampeni yao vizuri, lakini karibuni mambo yameanza kuwaendea vibaya.

Walifanikiwa kuwalaza Union Berlin, lakini wakashindwa na Einracht Frankfurt katika pambano la Bundesliga, baadaye walitoka sare 2-2 na Borussia Monchengladbach, kabla ya kushindwa na Frankfurt kwa mara ya pili, lakini katika pambano la DFB Cup.

Walikaza na kutoka sare 0-0 na wapinzani wao wakuu, Bayern Munich kabla ya kurejea na makali na kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Weder Bremen.

Ushindi mwembamba wa 2-1 dhidi ya Benfica uliwapa matumaini makubwa katika mchujo wa makundi, lakini mambo yakaharibika walipochapwa 2-0 nna Lyon.

Walirejea kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Zenith St Petersburg kabla ya kuandikisha ushindi wa 2-0 dhidi ya klabu hiyo ya Urusi.

Walifuzu kwa maondoano kufuatia sare ya 2-2 dhidi ya Benfica na Lyon, mtawaliwa.

Lakini huenda wakatatizika leo usiku dhidi ya Spurs ambao kikosi chao kimeimarika licha ya kukosa wachezaji kadhaa muhimu wanaouguza majeha.

Katika mechi nyingine ya UEFA, Atalanta ya Italia itakuwa nyumbani kupepetana na Valencia ya Uhispania huku ikijivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi nne za Ligi Kuu ya Italia.

Valencia wataingia uwanjani bila beki wao wa katikati.