Spurs watinga hatua ya 16-bora ya Europa League baada ya kubandua Wolfsberger ya Austria kwa mabao 8-1

Spurs watinga hatua ya 16-bora ya Europa League baada ya kubandua Wolfsberger ya Austria kwa mabao 8-1

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur walitinga hatua ya 16-bora ya Europa League msimu huu baada ya kuwabandua Wolfsberger kutoka Austria kwa jumla ya mabao 8-1.

Hii ni baada ya kiungo Dele Alli kuongoza waajiri wake Tottenham kusajili ushindi wa 4-0 katika mchuano wa mkondo wa pili mnamo Februari 24, 2021, nchini Uingereza.

Chini ya kocha Jose Mourinho, Tottenham walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wa maruadiano wakijivunia ushindi wa 4-1 katika mchuano wa awali katika mkondo wa kwanza.

Alli aliwafungulia Tottenham karamu ya mabao katika dakika ya 10 kabla ya kuchangia mengine mawili yaliyofumwa wavuni na Carlos Vinicius almaarufu Alves Morais katika dakika za 50 na 83 mtawalia.

Ingawa hivyo, kiungo huyo raia wa Uingereza anahusishwa na uwezekano wa kuagana na Tottenham msimu huu na kutua kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) ya kocha Mauricio Pochettino mwishoni mwa msimu huu. Goli la nne la Tottenham lilifumwa wavuni na Gareth Bale katika dakika ya 73.

Kufikia sasa, hakuna timu katika Uefa Cup ambayo imewahi kubatilisha matokeo ya kichapo cha mabao matatu na zaidi kwenye mkondo wa kwanza nyumbani na kupiga hatua kwenye kipute hicho.

Hivyo, Wolfsberger walitua nchini Uingereza kurudiana na Tottenham wakifahamu ukubwa wa kibarua kilichokuwa mbele yao.

Tottenham wangalifunga idadi kubwa zaidi ya mabao ila makombora mazito ya Vinicius aliyemtatiza pakubwa beki Gustav Henriksson yalipanguliwa kirahisi na kipa Manuel Kuttin.

Masogora wa Mourinho kwa sasa wanatarajia kufahamu mpinzani wao katika hatua ya 16-bora baada ya droo ya hatua hiyo itakayofanywa mnamo Ijumaa ya Februari 26, 2021.

Hadi waliposhuka dimbani kwa mchuano wa mkondo wa pili dhidi ya Wolfsberger, Tottenham walikuwa wamepigwa mara tano kutokana na michuano sita ya EPL. Kwa kuwa mbio za kuwania ufalme wa EPL zimefikia ukingoni mwa kikosi cha Mourinho, mkufunzi huyo wa zamani wa Real Madrid, Chelsea na Manchester United bado ana fursa ya kushindia waajiri wake taji la kwanza baada ya miaka 13 muhula huu.

Zaidi ya kufukuzia taji la Europa League, Tottenham tayari wamefuzu kwa fainali ya Carabao Cup ambapo wanatarajiwa kukutana na Manchester City mnamo Aprili 25, 2021 uwanjani Wembley, Uingereza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Pep ataka Manchester City wawe katili zaidi licha ya...

AKILIMALI: Kijana hodari wa uchoraji aliyejigundua kwenye...