Michezo

Spurs wavunja benki na kusajili beki Sergio Reguilon

September 21st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wamekamilisha usajili wa beki matata raia wa Uhispania, Sergio Reguilon ambaye ameagana rasmi na Real Madrid na kutia saini mkabata wa miaka mitano ambao umerasimishwa kwa kima cha Sh3.8 bilioni.

Reguilon, 23, alipokezwa malezi ya soka katika akademia ya Real na aliwajibishwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha watu wazima mnamo Oktoba 2018.

Hadi alipojiunga na Tottenham, alikuwa amechezea Sevilla ya Uhispania kwa mkopo wa msimu mmoja wa 2019-20. Katika kipindi hicho, aliwasaidia Sevilla kutwaa ubingwa wa Europa League na kutinga nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Ingawa Reguilon alihusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Manchester United, Tottenham waliwapiga kumbo na kujinasia huduma za beki huyo ambaye anatazamiwa kushirikiana na Matt Doherty aliyetokea Wolves na kuwa tegemo kubwa katika kikosi cha kocha Jose Mourinho.

Reguilon atavalia jezi nambari tatu mgongoni kambini mwa Tottenham.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO