SRC yalenga kupunguza marupurupu ya watumishi wa umma

SRC yalenga kupunguza marupurupu ya watumishi wa umma

PETER MBURU na CHARLES WASONGA

MAPATO ya wafanyakazi wa umma yatapungua kuanzia Julai 2021 sera ya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kuhusu upunguzaji wa marupurupu itakapoanza kutekelezwa.

Mwenyekiti wa tume hiyo Lyn Mengich Jumatatu alisema chini ya mabadiliko yanayopendekezwa katika sera hiyo SRC itahakikisha kuwa marupurupu ambayo wafanyakazi wa umma watapokea hayazidi asilimia 40 ya mishahara yao.

“Wakati huu, kwa wastani, marupurupu ya wafanyakazi wa umma ni sawa na asilimia 48 ya mishahara yao. Lakini tuna taasisi za umma ambazo hulipa marupurupu ya hadi asilimia 100 au hata zaidi ya mishahara ya watumishi wa umma. Kwa hivyo, hali ni tofauti baina ya taasisi mbalimbali za serikali,” Bi Mengich akawaambia wanahabari katika hoteli ya Hilton, Nairobi.

Bi Mengich alisema sera ya marupurupu na mafao katika sekta ya umma – Draft Allowances and Benefits Policy for the Public Sector – inahakikisha baadhi ya marupurupu yanaunganishwa na mengine kufutuliwa mbali.

“Ili kufikia lengo hili, tunapendekeza kuainisha marupurupu kwa kategoria tano muhimu, nazo ni marupurupu ya nyumba, marupurupu ya usafiri, marupurupu yanayohusiana na kazi, marupurupu yanayohusiana na wajibu fulani wa mfanyakazi, na marupurupu yanayohusiana na masuala ya leba,” akaeleza.

Bi Mengich alisema SRC imetambua kuwa wakati huu, wafanyakazi katika sekta ya umma wanapokea jumla ya marupurupu 247.

“Mnamo 1999 wafanyakazi wa umma walikuwa wakilipwa marupurupu 31 pekee. Marupurupu haya yaliongezeka hadi 156 serikali ya Jubilee ilipoingia mamlakani. Ongezeko la marupurupu linatokana na hali kwamba aina moja ya marupurupu hupewa majina tofauti,” akasema.

“Kwa hivyo, ili kuzima hali kama hii, marupurupu ambayo yamekuwa yakitolewa kwa shughuli sawa lakini yamepewa majina tofauti, yataunganishwa na kupewa jina moja. Na marupurupu mengine yasiyo na msingi wowote yanaondolewa kabisa,” Bi Mengich akaeleza.

Mwenyekiti huyo alisema sera hiyo inalenga kupunguza gharama ya ulipaji mishahara serikalini kutoka kima cha Sh100 bilioni kwa mwaka, kutoka Sh827 bilioni hadi Sh727 bilioni.

“Inasikitisha kuwa wakati huu, gharama ya ulipaji marupurupu pekee katika sekta ya umma ni Sh322 bilioni. Sera hii mpya inalenga kupunguza gharama hii kwa angalau Sh100 milioni,” Bi Mengich akasema.

SRC imesema asasi mbalimbali za serikali kuu na zile za kaunti zitapewa muda wa miezi sita, kuanzia Julai 1, 2021, kutekeleza sera hii mpya kuhusu marupurupu.

You can share this post!

Kassim Majaliwa aendelea kuonyesha umahiri Zanzibar...

KMPDU yaahidi kufanya hamasisho wahudumu wa afya wapokee...