SRC yazima nyongeza ya mishahara katika sekta ya umma

SRC yazima nyongeza ya mishahara katika sekta ya umma

Na CHARLES WASONGA

RAIS, Naibu Rais, Mawaziri, Wabunge, maafisa wakuu serikalini na watumishi wa umma hawatapata nyongeza ya mishahara kwa miaka miwili kutokana na hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la corona.

Mwenyekiti wa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) Lyn Mengich, Alhamisi alisema hatua hiyo imetokana na ombi kutoka kwa Hazina ya Kitaifa iliyoiomba kwamba iahirishe nyongeza ya mishahara hadi uchumi utakapoimarika.

“Japo tumechunguza upya mishahara na marupurupu ya wafanyakazi wa umma, hakutakuwa na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wote wa umma. Hazina ya Kitaifa iliomba kwamba juhudi zote zielekezwe katika mchakato wa ufufuzi wa uchumi ulioathiriwa na janga la Covid-19. Kwa hivyo, hakutakuwa na nyongeza ya mishahara katika miaka ya kifedha ya 2021/22 hadi 2022/23,” Bi Mengich akawaambia wanahabari Alhamisi katika hoteli ya Hilton, Nairobi.

Mwenyekiti huyo wa SRC hata hivyo alifafanua kuwa shughuli nyingine zozote za usawazishaji wa mishahara katika sekta ya umma zitaendelea kufanyika ndani ya bajeti zilizotengwa.

Bi Mengich alisema hatua hiyo ya kuzima nyongeza ya mishahara itaokoa Sh82 bilioni kila mwaka ambazo zitaelekezwa katika shughuli nyingine za ufufuzi wa kiuchumi.

You can share this post!

Beki Danny Rose ajiunga na Watford baada ya kuagana na Spurs

Saa za kafyu zaongezwa kaunti 13 zilizoko Magharibi, Nyanza