Michezo

Ssimbwa ajiuzulu akilalamikia wachezaji kumgomea

April 9th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI wa Batoto Ba Mungu, Sam Ssimbwa amejiuzulu nafasi ya kocha mkuu Jumapili.

Kocha huyo mzaliwa wa Uganda aliamua kugura kazi hiyo kufuatia kichapo cha 2-1 mikononi mwa Thika United ambayo imedhalilishwa mno katika Ligi Kuu ya Kenya.

Mwenyekiti wa Sofapaka Elly Kalekwa amethibitisha habari hizo, akisema Ssimbwa aliomba kujiondoa akilalamikia tabia ya wachezaji kutojituma kwa mechi ili wamuaibishe.

 

“Amejiuzulu. Amewapa wachezaji buriani ya kuonana na tunaheshimu hilo. Anadai kuwa wachezaji wanamgomea, hawataki kusikiza anachosema,” akasema.

“Hakuna haja kwake kuandika barua ya kujiuzulu, tumekubali uamuzi wake.”

“Hakuna uhusiano mbaya kati yetu naye, jinsi amesema mwenyewe, atasalia kuwa mwandani na kututakia mema kwa mechi,|” akaongeza.

 

Kufikia sasa, Sofapaka imeshinda mechi tano, ikapata sare moja na kulimwa mechi tatu.