Michezo

St Georges ya Ethiopia yaongezea hela kupata huduma za Mieno

January 9th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MIBABE wa soka nchini Ethiopia St Georges wameimarisha juhudi za kumsaini kiungo wa Gor Mahia Humphrey Mieno kwa kuwasilisha ofa nene zaidi baada ya ile ya awali ya Sh1.5milioni kukataliwa.

Taarifa za kuaminika zinadai kwamba ingawa K’Ogalo walikatalia mbali ofa ya awali, waliwaeleza St Georges kwamba wapo tayari kumwaachilia kiungo hiyo iwapo pesa hizo zingeongezwa.

“Gor Mahia walikataa ofa ya awali kwa kuandikia usimamizi wa St. Georges wakisema wapo tayari kwa majadiliano pesa zikiongezwa. Klabu hiyo sasa imerejea na ofa ya kudondoshewa mate ambayo indaiwa itakuwa mara mbili ya ile ya awali. Ni muda tu kabla ya pande zote mbili kukubaliana,” ikatanguliza taarifa hiyo.

“Gor Mahia imeonyesha nia ya kumruhusu mchezaji huyo aondoke ndiposa wameanzisha upya mazungumzo  na St George. Ni muda tu kabla ya uhamisho kukamilishwa,” ikahitimisha taarifa hiyo.

Kiungo huyo wa zamani wa Sofapaka na Tusker hajawajibikia Gor Mahia katika mechi tatu zilizopita huku ikisemekana amekuwa akisukuma sana uongozi wa Gor Mahia kukamilisha mchakato wa uhamisho wake hadi St Georges.

Gor watavaana na Posta Rangers Jumatano Januari 9, 2019 kwenye mechi ya Ligi Kuu nchini(KPL) kabla ya kuialika New Star ya Cameroon katika mechi ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho(CAF) Jumapili Januari 13 ugani MISC Kasarani.