STAA WA SPOTI: Rayton ‘Boom Boom’ Okwiri atamba ndondi za kulipwa bara Afrika

STAA WA SPOTI: Rayton ‘Boom Boom’ Okwiri atamba ndondi za kulipwa bara Afrika

NA CHARLES ONGADI

RAYTON ‘Boom Boom’ Okwiri ni kati ya mabondia nchini waliopata mafanikio makubwa katika mchezo huu ulio na mashabiki kibao duniani.

Okwiri, 37, mzaliwa wa Butere, Kakamega anatarajiwa kupanda ulingoni Juni 30 kuchubuana sura na Emmany Mukuna Kalombo maarufu kama ‘ The General ‘ raia wa DRC.

Pigano hili litakuwa ni la kuwania taji lililo wazi la IBF International katika uzito wa Super welter ambapo endapo Okwiri atafaulu kumdengua Kalombo, atapata fursa ya kuwania taji la dunia la IBF.

“ Naendelea kujiandaa nikiwa na wingi wa matumaini ya kupata ushindi dhidi mpinzani wangu nchini Afrika kusini,” asema mwamba huyu wa masumbwi nchini.

Kabla ya kujitosa katika ngumi za kulipwa mwaka 2017, Okwiri alitamba kinyama katika ngumi zisizo za malipo akiishindia taifa medali kibao.

Mshawasha wa kujiunga na ndondi ulianza kumvaa kipindi akiwa mwanafunzi wa shule ya upili ya Serani Mombasa mwaka wa 2003.

Okwiri alianza kuinukia akiwa kwenye klabu ya KPA kabla ya kusajiliwa katika idara ya Magereza akicheza katika uzito wa welter ambapo alitawala Afrika Mashariki na hata bara la Afrika kwa kipindi kirefu.

Baada ya kupata mafanikio makubwa katika ndondi zisizo za malipo, mwaka wa 2009, alichaguliwa kushiriki mashindano ya AIB Pro boxing na kutamba akiwanyuka kati ya mabondia hodari duniani kama Audrey Zamkovoy wa Urusi.

Hata hivyo, nyota ya Okwiri ilianza kung’aa kama mbalamwezi mara aliposhinda medali ya dhahabu katika mashindano ya bara la Afrika ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka wa 2016.

Ushindi huo ulimwezesha kufuzu kushiriki kwa Michezo ya Olimpiki yaliyoandaliwa Rio de Jeneiro nchini Brazil mwaka wa 2016.

Licha ya kutovuna medali katika mashindano hayo, mchezo wake uliwavutia wadhamini kibao wa masumbwi duniani walioanza kumsaka wakilenga kumsajili katika kampuni zao.

Alijitosa kwa mara ya kwanza katika masumbwi ya kulipwa mwaka wa 2017 na kumnyuka Swalehe Mkalekwa wa Tanzania.

Okwiri alishinda taji lake la kwanza katika ngumi za kulipwa baada ya kumshinda Hussein Itaba wa TZ na kutwaa taji la Africa Boxing Union (ABU) katika uzito wa Middle mwaka wa 2019.

Katika kuonesha upendo wake kwa taifa, Okwiri aliweza kuwachilia ukanda wake na kuamua kuwakilisha taifa katika mashindano ya kufuzu kushiriki Michezo ya Tokyo Olimpiki yaliyoandaliwa Dakar, Senegal.

Kufikia sasa, Okwiri amepigana mara tisa na kushinda mapigano nane huku akishinda sita kati yazo kwa njia ya KO na hajatolewa kamasi na yeyote huku akiandikisha matokeo ya sare mara moja.

  • Tags

You can share this post!

MATUKIO MUHIMU: Amefuzu ukocha viwango vya Fifa, KNVB na...

Staa Lewandowski bado yupo Bayern Munich hadi 2023

T L