Habari Mseto

Starehe Boys yajitetea kumkataa mwanafunzi aliyepata 417 KCPE

January 23rd, 2019 1 min read

Na Valentine Obara

SHULE ya Upili ya Wavulana ya Starehe imetetea uamuzi wake wa kumkataa mwanafunzi aliyeteuliwa na serikali kujiunga na shule hiyo kwa Kidato cha Kwanza.

Kaimu Mkurugenzi wa shule hiyo, Bw Josphat Mwaura alisema ingawa wamejitolea kushirikiana na serikali katika mfumo mpya wa uteuzi wa wanafunzi waliohitimu katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE), Starehe ina haki ya kutimiza kikamilifu sheria zake za ndani zinazotumiwa kuamua wanafunzi wanaostahili kukubaliwa kujiunga na shule hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Wizara ya Elimu ililazimika kumtafutia mwanafunzi huyo aliyepata alama 417 kwenye KCPE nafasi katika Shule ya Upili ya Mangu baada ya wasimamizi wa Starehe kusisitiza hakutimiza matakwa yaliyohitajika licha ya kupewa nafasi hiyo na serikali.

Wasimamizi wa Starehe walizidi kudai babake mwanafunzi huyo, Bw David Babu, alikataa kufuata ushauri wao. Kulingana na Bw Mwaura, shule hiyo iliyo katika Kaunti ya Nairobi ilipokea majina ya wanafunzi 24 na 23 kati yao walichukuliwa baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa.