Michezo

Starehe Foundation FC yatwaa kombe la NG-CDF Thika

December 21st, 2020 1 min read

LAWRENCE ONGARO

STAREHE Foundation FC ilionyesha ujabali wake kwa kuicharaza Destiny FC kwa mabao 5-3 kupitia mikwaju ya matuta baada ya kumaliza muda wa kawaida wakiwa sare ya 1-1.

Mechi hiyo ya Jumapili ilikuwa fainali ya kuwania kombe la hazina ya ustawi wa eneobunge, NG-CDF, ya Thika katika Uwanja wa chuo cha Thika Technical College.

Katika fainali ya wanadada klabu ya Kiambu Ladies FC iliibwaga Green Commandos Ladies FC kwa mabao 2-0.

Wafungaji walikuwa Jane Njeri dakika ya 28 na Mary Muthoni dakika ya 72.

Mashindano hayo yalijumuisha timu 98 za wavulana huku 12 zikiwakilisha wanadada.

Michuano hii iliyodhaminiwa na mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina iligaragazwa katika viwanda vya Umoja na Kiboko kabla ya kucheza fainali katika uwanja wa Thika Technical.

Starehe Foundation chini ya kocha Macharia Gathu ilipata mabao kupitia kwa Brian Misago, David Kiki, Joseph Kinuthia, Denis Okoth, na Briton Ngige.

Kwa upande wa Destiny wafugaji walikuwa Joseph Maina, George Otieno, na Peter Macharia.

Washindi upande wa wavulana walipokea kombe, jezi, mpira, na pesa taslimu Sh75,000. Vijana wa Destiny waliridhika na Sh50,000, jezi, na mpira pamoja na medali.

Timu zingine zote zilizoshiriki zilipokea kati ya Sh10,000 na 20,000 pamoja na jezi na mipira.

Mdhamini wa mashindano hayo Wainaina, aliridhika na jinsi vijana hao walivyoonyesha vipaji vyao.

“Nimeridhika na jinsi vijana hao walivyoonyesha ubora wao wa kusakata gozi. Kwa hivyo mashindano hayo yatakuwa yakiendelea kila mara ili vijana wawe na jambo muhimu la kufanya,” akasema mbunge huyo.

Alitoa wito kwa vijana wote wanaoelekea kusherehekea sikukuu ya Krismasi wawe makini na maisha yao hasa akiwataka wasijiingize katika mambo maovu.

Alipendekeza serikali iongeze fedha za mgao wa hazina ya NG-CDF na kiwango cha Sh10 milioni zaidi ili kuinua michezo mashinani.