Habari

Starehe Girls yafungwa baada ya kugundulika visa vya ugonjwa usiojulikana

October 3rd, 2019 1 min read

Na SARAH NANJALA na OUMA WANZALA

MAAFISA wa Wizara ya Elimu na bodi ya usimamizi wa shule ya Starehe Girls Centre, wameifunga baada ya kugundulika visa vya dalili za ugonjwa ambao haujatambulika.

Uamuzi huo unajiri baada ya maafisa hao na wakuu wa shule hiyo kukutana kwa dharura leo Alhamisi baada ya wanafunzi 52 kutengwa wakiwa na dalili za ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa Elimu Kanda ya Nairobi, Jared Obiero amesema matarajio ni kwamba shule hiyo itafunguliwa tena Jumatatu, Ocktoba 7.

Wanafunzi wanaougua ugonjwa huo wameonyesha dalili mbalimbali zikiwemo kukohoa sana, kupiga chafya na mafua ya kiwango cha chini, kulingana na taarifa ya Jumatatu kutoka kwa shule hiyo.

Wataalamu wa afya kutoka Idara ya Kushughulikia Umulikaji wa Maradhi Kidharura wamechukua sampuli ili kufanya uchunguzi na utafiti katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kimatibabu Nchini (Kemri).

Matokeo yalitarajiwa leo Alhamisi, lakini shule haijaweka wazi kwa wazazi na umma.

Wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya, Kaunti ya Nairobi na madaktari wa kujitolea kutoka jumuiya ya Starehe wanachunguza hali shuleni humo.