Michezo

Starlest tayari kupigana na Black Queens kufuzu Olimpiki

October 3rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets imekamilisha mazoezi uwanjani Accra tayari kwa mechi ya kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki dhidi ya Black Queens nchini Ghana mnamo Oktoba 4, 2019.

Taarifa kutoka jijini Accra zimesema kuwa Starlets ya kocha David Ouma ilipata fursa ya kufanyia mazoezi katika uwanja huu unaobeba mashabiki 40,000 mnamo Alhamisi alasiri saa za Ghana.

Kabla ya kuelekea Accra mnamo Oktoba 1, Ouma pamoja na nahodha Dorcas Shikobe na mvamizi nyota Mwanahalima Adam walisema Kenya italenga kudhibiti Black Queens.

Licha ya kuwa na rekodi mbaya, warembo wa Ouma wanaamini wanaweza kupata matokeo mazuri ugenini kabla ya kurejea jijini Nairobi kumaliza kazi mnamo Oktoba 8.

Starlets ililemewa 3-1 ilipokutana na Ghana katika mechi ya makundi ya Kombe la Afrika mwaka 2016 nchini Cameroon kabla ya kutoka 1-1 katika mechi ya kirafiki mwaka 2018 uwanjani Kasarani jijini Nairobi.

Kikosi cha Kenya: Makipa – Annette Kundu (Eldoret Falcons), Judith Osimbo (Gaspo Women); Mabeki – Dorcas Shikobe (Oserian Ladies), Vivian Nasaka (Vihiga Queens), Wincate Kaari (Gaspo Women), Lydia Akoth (Thika Queens), Quinter Atieno (Gaspo Women), Nelly Sawe (Thika Queens), Ruth Ingosi (Eldoret Falcons); Viungo – Corazone Aquino (Gaspo Women), Sheryl Angach (Gaspo Women), Jentrix Shikangwa (Wiyeta Girls), Topister Nafula (Vihiga Queens), Janet Moraa (Eldoret Falcons), Elizabeth Wambui (Gaspo Women), Cynthia Shilwatso (Vihiga Queens), Elizabeth Katungwa (Kwale Girls); Washambuliaji – Mwanalima Adams (Thika Queens), Mercy Airo (Kisumu All Starlets), Bertha Omita (Kisumu All Starlets).