Michezo

Starlets kujiandalia mchujo wa Olimpiki dhidi ya Ethiopia

August 17th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets imejawa na matumaini italima Ethiopia katika mechi ya kirafiki leo Jumamosi uwanjani Kenyatta mjini Machakos huku ikitupia jicho kwa mechi ya kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki dhidi ya Malawi mnamo Agosti 28.

Starlets ilipigwa na Ethiopia 1-0 zilipokutana mara ya mwisho Julai 7 mwaka 2018 katika mechi ya soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) nchini Rwanda.

Kenya inaorodheshwa katika nafasi ya 141 duniani katika viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) nayo Ethiopia ni ya 118.

Inamaanisha kuwa Kenya ikipata ushindi dhidi ya Ethiopia itaelekea jijini Blantyre kwa mechi ya raundi ya pili ya mkondo wa kwanza ikiwa na motisha dhidi ya nambari 146 duniani Malawi.

Kenya na Ethiopia ziliimarisha maandalizi yao uwanjani Kenyatta, Ijumaa.

Starlets haijacheza mechi kwa muda mrefu tangu masaibu yake ya kuingia Kombe la Afrika (AWCON) baada ya kushtaki Equatorial Guinea mwaka 2018 na kuondolewa kabla ya mashindano hayo kuanza.

Ilikaba Black Queens ya Ghana 1-1 uwanjani Kasarani mnamo Novemba 7, siku chache tu kabla ya kupokonywa tiketi iliyorejeshewa Equatorial Guinea.

Malawi, ambayo ilirejelea mazoezi yake baada ya kushiriki soka ya Afrika ya Kusini (Cosafa) nchini Afrika Kusini zaidi ya wiki moja iliyopita, itazuru Nairobi kwa mechi ya marudiano mnamo Agosti 31.