Michezo

Starlets na She-polopolo zanoa kucha kukabiliana mjini Kitwe

March 16th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets ya Kenya na She-polopolo ya Zambia zimeimarisha mazoezi kabla ya kuvaana katika mechi ya kirafiki mjini Kitwe hapo Machi 25, 2018.

Starlets ya kocha Richard Kanyi imekita kambi mjini Machakos kujinoa uwanjani Kenyatta nayo She-polopolo inafanyia mazoezi yake mjini Kitwe.

Mara ya mwisho Starlets ilikabiliana na She-polopolo ni mwaka 2012 katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la Under-20.

Kenya ilizimwa 2-1 jijini Lusaka kabla ya kuabisha Wazambia 4-0 katika mechi ya marudiano uwanjani Nyayo jijini Nairobi katika raundi ya kwanza. Mechi hizo zilisakatwa kati ya Februari 17 na Machi 3, 2012.

Kabla ya kunyamazisha Zambia, Starlets ilikuwa imebandua nje Lesotho kwa jumla ya mabao 4-2 katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza baada ya kukabwa 2-2 nyumbani kabla ya kutawala ugenini 2-0 kati ya Oktoba 28 na Novemba 19, 2011.

Kampeni ya Kenya kuingia Kombe la Dunia mwaka 2012 ilikatizwa na Tunisia katika raundi ya pili ilipolazwa 2-1 nyumbani na ugenini.

Starlets na She-polopolo zinajiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika litakaloandaliwa nchini Ghana kutoka Novemba 17 hadi Desemba 1, 2018. Kenya italimana na Uganda mnamo Aprili 4 (nyumbani) na kuelekea ugenini Aprili 7.

Mshindi kati ya Kenya na Uganda baada ya mikondo yote miwili atakabana koo na mabingwa wa zamani Equatorial Guinea katika raundi ya pili kati ya Juni 4 na Juni 12, 2018.

Mshindi wa raundi ya pili ataingia katika Kombe la Afrika na kupata fursa ya kuwania mojawapo ya tiketi tatu za kushiriki Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Ufaransa mwaka 2019.