Michezo

Starlets watupwa nje ya AWCON

November 16th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi Harambee Starlets ya Kenya iko nje ya soka ya Kombe la Afrika la wanawake (AWCON) mwaka 2018 baada ya rufaa yake kutupiliwa mbali na mahakama ya kusikiza michezo (CAS) mjini Lausanne nchini Uswizi, Ijumaa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Novemba 16, 2018, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limetakia washiriki kila la kheri na kuongeza kwamba halitachoka kutafuta haki.

“Tuliomba mahakama ya CAS kushurutisha Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) lijumuishe Kenya katika mashindano ya AWCON ama iyasimamishe kabisa hadi uamuzi unaofaa ufanywe. Tulikuwa na kibarua kikubwa, ingawa tuliamini katika nguvu za kesi tuliyowasilisha.

“Uamuzi wa mwisho uliofanywa na Rais wa Kitengo cha Rufaa hata hivyo ni kukataa ombi letu na tunaelewa na kuheshimu uamuzi wa CAS.

“Hii, hata hivyo, haimaanishi kwamba huu ndio mwisho wa kesi. Rufaa yetu dhidi ya CAF bado iko wazi, na tutaendelea kupigana kuona haki inatendeka ili kurekebisha madhara ambayo timu yetu ya Starlets na watu wa Kenya wamefanyiwa.

“Tutaendelea kutafuta haki katika mahakama ya CAS ili kuthibitisha kwamba kama shirikisho na kama Wakenya hatutakaa kitako na kukubali uvunjaji wa sheria zinazodhuru timu zetu kuendelea.

“Kwa wakati huu, tunachukua fursa hii kutakia washiriki wa AWCON kila la kheri, na tuna uhakika kwamba Ghana itaendelea kuandaa mashindano mazuri bila sisi kuwepo na tutajiandaa vilivyo kuhakikisha Kenya inawakilishwa katika makala yajayo ya AWCON,” FKF imesema kupitia Afisa wa Mawasiliano, Barry Otieno.

Kenya ilikuwa imejumuishwa katika mashindano haya ya mataifa mwezi Oktoba baada ya kufaulu katika kesi yake dhidi ya Equatorial Guinea kuchezesha mchezaji ambaye FKF iliamini ni raia wa Cameroon.

Hata hivyo, ilipata pigo majuma machache yaliyopita pale CAF, ambyo ilikuwa imepiga Equatorial Guinea marufuku na kuipa Kenya tiketi ya kuwa katika AWON mwezi huu, ilibatilisha uamuzi na kurejeshea timu hiyo kutoka Afrika Magharibi tiketi na kuondoa Kenya kwenye orodha ya washiriki.

Mashindano ya AWCON yatatumika kuchagua wawakilishi watatu wa Bara Afrika katika Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Ufaransa mwaka 2019. Equatorial Guinea haiwezi kufuzu kwa sababu ilipigwa marufuku na Shirikisho la Soda Duniani (FIFA) kutokana na kutumia wachezaji ambao si raia wa nchini hiyo.