Michezo

Stars kufahamu Ijumaa wapinzani wake wa mechi za kirafiki

April 16th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limefichua kwamba timu ambazo Harambee Stars itapimana nazo nguvu kabla ya kuelekea nchini Misri kwa Kombe la Afrika (AFCON) 2019 zitafahamika Aprili 19.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka nchini Uhispania, Rais wa FKF Nick Mwendwa ameambia Taifa Leo kwamba wapinzani wa Kenya katika mechi hizo za kirafiki zitakazosakatwa Juni 7 na Juni 17 wanasalia siri kwa sasa hadi pale mazungumzo yatakapokamilika.

“Kufikia Ijumaa tutakuwa tumekamilisha mipango yote ya maandalizi ya Harambee Stars halafu tuwafahamishe sehemu ambayo tutafanyia mazoezi pamoja na timu tutakazotumia kujipima nguvu. Narejea jijini Paris siku ya Alhamisi baada ya kuzuru Uhispania kuona vijana wetu katika mashindano ya soka ya Under-16 (MIC Cup),” amesema.

Kenya inarejea katika AFCON baada ya kuwa nje miaka 15. Imetiwa katika Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na Tanzania. Senegal, Algeria, Kenya na Tanzania zinashikilia nafasi za 23, 70, 108 na 131 duniani, mtawalia.

Kocha wa Kenya, Sebastien Migne anatarajiwa kutaja kikosi cha AFCON mapema mwezi Mei. Wachezaji 26 kisha wataelekea Ufaransa kwa kambi ya mazoezi ya wiki tatu Mei 23. Mfaransa Migne atachuja wachezaji watatu kabla ya kuenda Misri.

RATIBA YA KENYA YA AFCON 2019

Mei 23: Harambee Stars yaelekea Ufaransa kwa kambi ya mazoezi ya wiki tatu

Juni 7: Mechi ya kwanza ya Kenya ya kirafiki

Juni 15: Harambee Stars yafunga safari kuelekea Misri

Juni 17: Mechi ya mwisho ya Kenya ya kirafiki

Juni 23: Kenya na Algeria (mechi ya Kundi C ya AFCON 2019)

Juni 27: Kenya na Tanzania (mechi ya Kundi C ya AFCON 2019)

Julai 1: Kenya na Senegal (mechi ya Kundi C ya AFCON 2019)

Julai 5-8: Mechi za raundi ya 16-bora AFCON 2019

Julai 10-11: Mechi za robo-fainali AFCON 2019

Julai 14: Mechi za nusu-fainali AFCON 2019

Julai 17: Mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba AFCON 2019

Julai 19: Fainali ya AFCON 2019