Michezo

Stars kufufua uhasama dhidi ya Eritrea

December 16th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya wanaume ya Kenya, Harambee Stars, italimana na Eritrea katika mechi ya nusu-fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenge Cup) jijini Kampala nchini Uganda hapo Desemba 17.

Hii ni baada ya Eritrea kujikatia tiketi ya kukutana na Kenya baada ya kumaliza Kundi A katika nafasi ya pili kwa alama tano ilipolazimisha sare tasa dhidi ya Somalia katika mechi yake ya mwisho Jumapili.

Eritrea pia ilinufaika na Djibouti kulimwa 4-1 Jumapili. Eritrea na Djibouti ziliingia mechi hizo zao za mwisho za makundi zikiwa bega kwa bega kwa alama nne kila mmoja.

Stars ilitinga nusu-fainali kwa kushinda Kundi B kwa jumla ya alama tisa baada ya kupepeta Tanzania 1-0, Sudan 2-1 na Zanzibar 1-0.

Dhidi ya Eritrea, Kenya, ambayo itakuwa inakaribisha kocha mkuu Francis Kimanzi kwenye benchi la kiufundi baada ya kumaliza marufuku ya mechi mbili, itakuwa ikitafuta kulipiza kisasi.

Stars ilizabwa 2-1 jijini Nairobi na kulemewa 1-0 jijini Asmara katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2007. Hiyo ndio mara ya mwisho mataifa haya yalikutana.

Nusu-fainali nyingine itakuwa katika ya Uganda, ambayo ilishinda mechi zake zote nne za makundi, itakabiliana na Tanzania iliokamilisha Kundi B katika nafasi ya pili.