Michezo

Sterling asifiwa kwa kuepusha City kuzama

October 3rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KUINGIZWA kwa Raheem Sterling katika kipindi cha pili kuliimarisha kikosi cha Manchester City ambacho kilikuwa kimelemewa vibaya na wapinzani wao, Dinamo Zagreb.

Mwingereza huyo aliwafungia bao ambalo pia lilikuwa lake la 10 katika mechi 12 alizochea mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nyota huyo alichangia pia katika kupatikana kwa bao la pili lililofungwa na Phil Foden dakika ya 95.

“Ni mchezaji muhimu kikosini. Amebarikiwa kipaji cha kung’ara wakati wowote,” Guardiola alisema kuhusu Sterling.

Akaongeza: “Anapenda kufunga mabao. Siku chache zilizopita alikiri kupoteza nafasi nyingi tulipocheza na Everton ingawa alifanikiwa kufunga moja. Nina hakika anaweza kuimarika zaidi na kufunga mabao katika mechi zijazo. Leo alimuandalia pasi nzuri Phil. Lakini itabidi awe mkali zaidi anapokaribia lango kufunga bao. Tunamshukuru kwa kuendelea kutufungia mabao kila anapopewa nafasi.”

Guardiola alikifanyia mabadiliko matano kikosi chake kilichocheza na Everton. Kevin De Bruyne hakucheza kutokana na jeraha– lakini huenda akawa kikosini Jumapili kucheza dhidi ya Wolves pamoja na Bernardo na David Silva.

Benjamin Mendy, João Cancelona na Sergio Agüero waliingia baadaye baada ya kuanza kama wachezaji wa akiba. Gabriel Jesus, Oleksandr Zinchenko na Kyle Walker hawakucheza.

Zagreb walikuwa wameshinda mechi zao zote kabla ya kichapo cha Jumanne usiku, lakini ilikuwa mechi yao ya 12 kushindwa katika Ligi ya Klabu Bingwa ugenini.

Mabeki wa katikati

Guardiola alianza safu ya ulinzi kwa kumpanga Fernandinho kushirikiana na Nicolás Otamendi kama mabeki wa katikati.

City walifanya mashambuliaji makali ambayo yalisababisha penalti, lakini mwamuzi akakataa baada ya Kévin Théophile-Catherine kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Juhudi za wachezaji kutaka mtambo wa VAR utumike kutoa uamuzi hazikufua dafu. Kwa mara nyingine, David Silva alifikiria alistahili kupewa penalti, lakini mwamuzi huyo, Serdar Gözübüyük akaamua upigwe mkwaju wa fri kiki.

Phil mwenye umri wa miaka 19 hajawahi kuchezea timu ya taifa ya Uingereza, lakini Sterling amesema kinda huyo ana kila sababu ya kuwa kwenye timu hiyo inayonolewa na kocha Gareth Southgate.