Stima, Rangers zagawanya pointi debi ya Mombasa

Stima, Rangers zagawanya pointi debi ya Mombasa

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

Coast Stima na Modern Coast Rangers FC zilitoka sare ya kufunga mabao 2-2 wakati wa mechi yao ya kusisimua ya dabi ya Mombasa ya Supaligi ya Taifa iliyochezwa uwanja wa Serani Sports, Jumamosi Machi 13, 2021.

Mchezo huo ulianza kwa kasi na Modern Coast ikiwa inafamnya mashambulizi ya mara kwa mara na kufanikiwa kuongoza kwenye dakika ya 20 wakati George Owiti alipopokea pasi nzuri kutoka kwa Juma Bakari kutuma kiki lililomshinda kipa wa Stima, Said Dhadho.

Ilikuwa katika kipindi cha pili ndipo Stima ilipoingia kwa kishindo na kusawazisha katika dakika ya 62 kupitia kwa Stephen Mwiti. Stima iliweza kujipatia bao la pili kwenye dakika ya 84 mfungaji akiwa Lucky Kaingu.

Rangers ilipigana kuhakikisha hawapotezi mchezo huo na ilikuwa katika dakika ya tatu ya majeruhi ndipo iliposawazisha kwa bao lilotingwa nyavuni na Rashid Nzau.

Kocha wa Coast Stima, Hussein Mlohammed alisema walistahili kushinda mechi hiyo lakini kwa kuwa ilikuwa ni dabi lolote hutokea. “Sisi tulikuwa bora zaidi na tuliongoza 2-1 kukiwa kumebakia dakika sita pekee lakini kosa dogo lilitunyima pointi zote tatu,” akasema Mohamed.

Kocha mwenzake wa Rangers, Mohamed Ahmed almaarufu Mohaa alisema alifurahishwa na jinsi wanasoka wake walivyopigana kuhakikisha hawatoki uwanjani mikono mitupu. “Ilikuwa karibu tupoteze pointi zote tatu lakini wachezaji walipambana kuhakikisha tunagawanya alama,” akasema Mohaa.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa minofu ya kuku iliyopakwa siagi

BURUDANI: Angie The Twerker ni mwigizaji mwenye talanta ya...