HabariSiasa

Stima zapotea, Ruto alazimika kununua jenereta na basi

October 24th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

NAIBU Rais William Ruto Jumatano alilazimika kununulia Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha KTTC, Nairobi jenereta na basi, baada ya stima kupotea mara mbili alipokuwa chuoni humo jenereta yake ilipokuchelewa kuwaka.

Stima zilipotea wakati Bw Ruto alikuwa akihutubia walimu wakuu wa vyuo vya TVET pamoja na washikadau wengine wa sekta hiyo nchini, huku akilazimika kusitisha hotuba kutokana na giza lililotawala jumba la mkutano.

Naibu wa Rais aliishia kupoteza takriban dakika kumi wakati wa visa hivyo, jambo lililoonekana kumkera na kukiri kwa vitendo wakati mkutano ulipoisha.

Japo aliendelea na mkutano baada ya jenereta kurekebishwa, baadaye alihakikisha kuwa amewacha suluhu ya aibu hiyo.

Alipomaliza na kuwahutubia wanafunzi wa chuo hicho ambao waliziba njia nje, Bw Ruto aliamrisha wizara ya elimu kununua jenereta mpya chuoni humo, na kuwasilisha humo ndani ya kipindi cha wiki mbili, ili kuondoa aibu hiyo tena.

Naibu Rais William Ruto apanda mti katika Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha KTTC, Gigiri, Nairobi Oktoba 24, 2018. Picha/ Peter Mburu

“Nimeamrisha wizara ya elimu kuleta jenereta mpya ndani ya kipindi cha wiki mbili ili ianze kufanya kazi baada ya yale tumeshuhudia huko ndani,” akasema Bw Ruto.

Lakini walipoona ukarimu wa naibu wa Rais, wanafunzi wa chuo hicho walichangamka na kumtaka pia awanunulie basi, ombi lililompata bila matarajio, lakini akalikubali na kusema atawanunulia.

“Nimeongea na mwalimu wenu mkuu na mtanunuliwa basi la ziada,” akasema baada ya kuzungumza kichinichini na mkuu wa chuo hicho.

Hatua yake iliwaacha wanafunzi wa chuo hicho wakishangilia, haswa kwa kuwa walikuwa wamezuiliwa kufika eneo la mkutano, lakini wakamzuia nje hadi awahutubie.

Alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa mtaala wa mafunzo ya kiufundi, alisema wakati umefika kwa mafunzo ya kiufundi kuchukuliwa kwa umuhimu zaidi kwani kwa muda mrefu watu wamekuwa wakidharau mafunzo hayo.