Habari Mseto

Stima zatoweka kortini kesi ya wakuu wa Kenya Power ikiendelea

July 18th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

TAA zilizimika ghafla Jumanne asubuhi katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi wakati kesi dhidi ya wakuu wa Kenya Power ilipokuwa ikiendelea.

Giza totoro lilikumba jengo lote la Mahakama na kutatiza shughuli za kusikizwa kwa kesi inayomkabili mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Dkt Ken Tarus, mtangulizi wake Ben Chumo na wakuu wengine.

Punde tu umeme ulipozimika, maafisa wa polisi walishika doria na kuwalinda washukiwa 24 waliokuwa kizimbani.

Kila mmoja katika mahakama aliamriwa atoke nje ikiwa ni pamoja na wanahabari waliokuwa wamesimama karibu na washtakiwa.

Mahakama ilijulishwa kuwa nyaya za stima ndizo zilisababisha hitilafu hiyo.

“Tumejulishwa kuwa hitilafu iliyopelekea nguvu za stima kupotea ilitokana na nyaya na wala sio kusababishwa na wafanyakazi wa Kenya Power ama kuzimwa kwa lengo la kutatiza kesi hii,” kiongozi wa mashtaka Alexander Muteti alisema.

Washtakiwa walikabiliwa na mashtaka ya kuruhusu kampuni ya Muwa kununua transfoma feki zinazosababisha kupotea kwa nguvu za umeme nchini kati ya Aprili 2012 na Juni 2018.

Baadaye jioni, washukiwa wote waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa taslimu baada ya kukaa korokoroni kwa muda wa siku nne.

Hakimu Mkuu Douglas Ogoti aliamuru washtakiwa wazuiliwe usiku katika kituo cha Polisi cha Gigiri wakijitayarisha kulipa dhamana na wale watashindwa wapelekwe gerezani leo.

Mbali na dhamana hiyo ya Sh1milioni, washtakiwa wote waliagizwa watie saini dhamana ya Sh3 milioni.

Washtakiwa pia walitakiwa wasiende katika afisi za KPLC. Pia waliamriwa wasiwasiliane na mashahidi kwa wakifanya hivyo dhamana zao zitafutiliwa mbali na wazuiliwe gerezani.

Washtakiwa pia watakuwa wanaripoti kwa afisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI) mara moja kila wiki hadi maagizo mbadala yatolewe.

Washukiwa wawili waliokuwa wakisakwa, Daniel Ochieng Muga na Bernard Githui Muturi walijisalamisha kwa korti jana na kuagizwa wafike kwa afisi ya DCI wachukuliwe alama za vidole na kuandikisha taarifa kisha wafike kortini Agosti 6 kusomewa mashtaka. Waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1milioni pesa taslimu.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 6.