Bambika

Stivo Simple Boy arudishiwa akaunti za kuvumisha muziki wake

May 17th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

BAADA ya pandashuka za hapa na pale alipokosana na meneja wake, mwanamuziki Stephen Otieno Adera almaarufu ‘Stivo Simple Boy’ amerudishiwa akaunti zake za kuvumisha muziki wake.

Hii ni baada ya meneja wake wa zamani, Chingiboy Mstado, kusema wamemaliza bifu baina yao.

Mstado alisema aliona msanii huyo angekuja kusumbuka siku za usoni akidai kuwa akaunti mpya zilizodaiwa kufunguliwa pia zilikuwa ni kupitia kwa mtu mwingine.

“Ni siku nyingi tangu tukae tusemezane hivi lakini nimefurahia kumuona tena, Mambo yalitokea na hasira pia zikapanda lakini nafikiri tulitafutana na nimeamua na roho yangu kwamba ni vizuri kumpa sapoti. Niliona bifu ya Sh150,000 si kitu kwangu,” alisema Mstado.

Akipiga stori na safu ya Bambika, Stivo alisema kuwa awali alikuwa na wasiwasi wa kupoteza mashabiki wake kwenye mitandao hiyo pamoja na kupoteza pato kupitia mtandao wa YouTube.

Msanii huyo ambaye alikuwa ameingiwa na kiwewe, tayari alikuwa ameazisha akaunti nyingine za mitandao ya kijamii kuvumisha na kusukuma kazi zake kwa mashabiki.

“Nilikuwa nimeanza kuambia mashabiki kunifuatilia kwenye akaunti mpya. Akaunti za kitambo zilikuwa na aliyekuwa meneja wangu, lakini sasa amenirudishia na mambo yako fiti,” akasema Stivo akiongeza kuwa “ndio manake”.

Bila kujitia jeuri, msanii huyo alieleza kuwa alihitajika kulipa kiasi fulani cha fedha ili kuzimiliki tena.

Ingawa hivyo, alilalamikia kile alidai ni kunyanyaswa wakati wa malipo ya kazi zake.

“Kufikia sasa tupo katika asilimia 90 ili kuzimiliki kabisa. Kuna kiasi kidogo cha fedha alidai tukamlipa ili kuzirejesha akaunti. Lakini, kuna pesa nyingi nimepoteza kwa kuwa hata akaunti ya YouTube nimegundua kuwa ilikuwa ikiingiza kati ya Sh60,000 na Sh70,000 lakini niliambiwa ilikuwa ikinilipa Sh10,000 kila mwezi,” alidai.

Aidha mwimbaji huyo alifichua kuwa yupo chini ya usimamizi mpya, mmoja wa mameneja wake, Geoffrey Machabe, akisajiliwa kuwa msanii wake.

Machabe alisema tayari wamepata rasmi shoo moja ambayo msanii Stivo anatarajiwa kupagawisha mashabiki wake.

“Mimi na Stivo ni marafiki tangu zamani. Mambo mengi yamefanyika lakini siko hapa kufanyia kama hapo awali. Pesa zote atakazolipwa na mteja ni zake,” aliahidi Machabe.

Mnamo Machi 2024, Stivo alisema kuondoka kwa meneja wake–Mstado–ndio sababu ya yeye kuanguka wakati wa kipindi cha burudani cha ‘10 Over 10’ kinachopeperushwa na runinga ya Citizen.

Akizungumza na mtangazaji nahodha wa kipindi hicho ’10 Over 10’ Azeezah Hashim, alidondoka na kuanguka ghafla.

Hali hiyo ilisababisha mabadiliko kwa dakika kadhaa, huku onyesho hilo likisitishwa kwa muda ili kuhakikisha kuwa mwanamuziki huyo anashughulikiwa.

Baada ya muda mfupi, habari ziliibuka kuwa alikuwa amerejewa na fahamu na alikuwa yuko katika hali nzuri.

Kabla ya kumpata meneja mpya, alikuwa ameambia Taifa Leo kwamba kuondoka kwa meneja wake wa zamani “huniletea mawazo mengi”.

“Kwa sasa niko sawa. Lakini huwa naishiwa na nguvu kwa kumkosa meneja wangu. Kuna watu walio na nia ya kutukosanisha,” alisema msanii huyo wakati huo.