Michezo

Straika Mitrovic wa Fulham apigwa marufuku mechi tatu kwa kumpiga kumbo mchezaji Ben White

June 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI wa Fulham, Aleksandar Mitrovic amepigwa marufuku ya mechi tatu kwa kosa la kumpiga kumbo mchezaji Ben White wakati wa mchuano wa Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Fulham waliibuka na ushindi wa 3-0 katika mechi hiyo.

Mitrovic, 25, alimpiga mwenzake kumbo kali la tumboni kimakusudi dakika tatu tu baada ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi kupulizwa uwanjani Elland Road.

Hata hivyo, Mitrovic aliepuka adhabu ya papo kwa hapo kwa kuwa refa Tony Harrington hakuliona tukio hilo.

Lakini sogora huyo mzawa wa Serbia alikiri kosa mnamo Jumatatu ya Juni 29, 2020, baada ya vinara wa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kurejelea video zilizonasa tukio hilo la rafu yake uwanjani.

Mitrovic ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa mabao katika kivumbi cha Championship hadi kufikia sasa msimu huu kwa mabao 23.

Fulham wamepoteza mechi zote mbili tangu kurejelewa kwa soka ya Uingereza mnamo Juni 17 tukio ambalo linawasaza masogora hao wa kocha Scott Parker katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama saba zaidi nje ya mduara wa vikosi vinavyopigiwa upatu kupandishwa ngazi hadi EPL mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Adhabu ambayo Mitrovic amepokezwa ina maana kwamba atakosa gozi la London Magharibi litakalowakutanisha waajiri wake na Queens Park Rangers (QPR) mnamo Juni 30, 2020, kisha mechi dhidi ya Birmingham City na Nottingham Forest.