Michezo

Straika Samatta amfuata Victor Wanyama EPL

January 22nd, 2020 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

NAHODHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta amemfuata Victor Wanyama wa Totttenham Hotspur katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mshambuliaji huyo ambaye amekuwa akichezea klabu ya Genk nchini Ubelgiji, amejiunga na Aston Villa kwa mkataba wa miaka minne na nusu uliogharimu Sh1 bilioni.

Hata hivyo, hakutarajiwa kuichezea Jumanne usiku dhidi ya Watford.

Kocha Dean Smith wa Villa akisaidiwa na John Terry, nahodha wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Uingereza, waliamua kumsajili Mtanzania huyo ili kujaza nafasi ya Wesley Moraes anayesumbuliwa na jeraha la goti.

“Sikutaka kutaja jina la mtu, lakini tumekuwa sokoni tukitafuta straika wa kuongezea kikosi nguvu kutokana na majeraha ya Wesley,” alisema Smith.

“Nimefurahi tumefanikiwa kumleta Mbwana hapa Aston Villa. Amekuwa akifunga mabao kama njugu msimu huu wote na tunatarajia mchango wake utaimarisha kikosi chetu,” kocha huyo aliongeza.

Samatta ameifungia Genk mabao 10 katika mashindano tofauti msimu huu, likiwemo bao muhimu alilotia kimiani dhidi ya Liverpool ugani Anfield, wakati wa pambano la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Straika huyo mwenye umri wa miaka 27 alitua saa chache tu baada ya Aston Villa kutangaza kuondoka kwa Johantahn Kodjia, aliyejiunga na klabu ya Al Gharafa ya Qatar kwa mkataba ambao haukuwekwa wazi.

Kadhalika, kocha Smith amemuachilia kipa Lovre Kalinic kujiunga na Toulouse ya Ufaransa kwa mkopo, kufuatia kuwasili kwa mkongwe Pepe Reina.

“Imebidi aondoke baada ya kufanikiwa kumpata Pepe, atakayesaidiana na Orjan Nyland ambaye amekuwa katika kiwango kizuri.”

“Kuna mechi kubwa zinakuja na lazima tujipange kabla ya wikendi wakati huu Wesley ni majeruhi na Davis Keinan hayupo. Safu ya mashambuliaji ni sehemu tunahitaji kuimarisha na tusipofanya hivyo, mambo yatakuwa mabaya kwetu,” aliongeza.

Tangu afunge bao katika mechi ya Klabu Bingwa dhidi ya Liverpool, ambayo klabu yake ilishindwa 2-1, Samatta amekuwa akiwaniwa na klabu kadhaa za EPL na sasa Villa imefaulu kunyakua huduma zake.

Kwa jumla, tangu atue Genk, Samatta ameifungia mabao 76 na kupiga pasi zilizochangia mabao 20 katika mechi 91 alizocheza.

Mtangulizi wake Victor Wanyama, ambaye ni nahodha wa Harambee Stars ya Kenya, alijiunga na Spurs akitokea Southampton mnamo 2016.