Michezo

Straika wa Real taabani kuhusu corona

March 24th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BELGRADE, Serbia

STRAIKA wa Real Madrid, Luka Jovic yuko taabani kwa kukiuka masharti ya karantini wakati huu wa janga la corona, aliposafiri kwenda kumtembelea mpenzi wake jijini Belgrade, Serbia.

Baba mzazi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 amesema kwamba, itamlazimu mwanawe huyo kukubali adhabu yoyote ikiwemo kufungwa jela, endapo atapatikana na hatia.

Jovic alisafiri kutoka Uhispania hadi Serbia wiki iliyopita kinyume cha kanuni za serikali ya Serbia katika juhudi za kudhibiti ueneaji wa virusi vya homa kali ya corona.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Rais wa Serbia, Aleksandar Vucic Jovic ameagiza vyombo vya usalama katika taifa hilo kuanzisha uchunguzi dhidi ya Jovic na kumchukuliwa hatua kali za kisheria iwapo itabainika kwamba kusafiri kwake kuliongeza viwango vya maambukizi ya corona.

Picha zilizopakiwa katika mitandao ya kijamii wikendi iliyopita zilionyesha Jovic akiandamana na mpenzi wake, Sofia Milosevic jijini Belgrade huku wakinasa video za kudhihirisha kukomaa kwa mahaba yao wakati mrembo huyo alikuwa akisherehekea siku ya kuzaliwa.

Kwa upande wake, Milan ambaye ni babake Jovic, amesisitiza kwamba picha hizo hazikupigiwa nchini Serbia bali Uhispania.

Ingawa hivyo, ameshikilia kuwa mwanawe yuko tayari kwa adhabu yoyote itakayopendekezwa na serikali ya Serbia.

“Kabla ya kusafiri, Jovic alifanyiwa vipimo mara mbili na kubainika hana virusi vya corona. Matokeo hayo yalimweka huru kufunga safari ya kuelekea Serbia kukutana na mchumba wake Sofia ambaye ni mjamzito,” akaeleza Milan.

“Hata hivyo, nakubaliana na hatua iliyochukulia na serikali ya Serbia. Kusafiri kwa Jovic ni kinyume na kanuni za nchi na anafaa kuadhibiwa kwa kosa hilo.”

Uhispania ndilo taifa la pili baada ya Italia kuathiriwa pakubwa na janga na corona barani Ulaya.

Ligi kuu La Liga kwa sasa imesitishwa kwa muda usiojulikana huku kikosi kizima cha Real kikitengwa baada ya mchezaji wao mmoja wa timu ya vikapu, ambaye alikuwa akiugua corona kutumia vifaa vya mazoezi vya timu ya soka.

Aidha, baadhi ya wafanyakazi wa Real walioathiriwa pia wametengwa na wanaendelea kutibiwa chini ya uangalizi wa maafisa wa afya wanaojitahidi kudhibiti viwango vya maambukizi.

Mbali na kifo cha rais wa zamani wa Real, Lorenzo Sanz, 76, na aliyekuwa kocha wa Atletico Portada Alta, Francisco Garcia, 21, janga la corona limewaathiri pia wachezaji kadhaa wa klabu ya Valencia.