Michezo

Strathmore yauma sakafu magongo

April 21st, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya magongo ya Chuo Kikuu cha Strathmore ‘Gladiators’ iliendelea kuandamwa na masaibu ilipolazwa mabao 3-2 na Sailors kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezewa City Park, jijini Nairobi Ijumaa.

Strathmore iliyotwaa taji hilo mwaka 2016 imejikuta pabaya ambapo imepoteza mechi tatu ilizocheza msimu huu.

Mwanzo wanazuo hao walipigwa na Western Jaguars kabla ya kulimwa bao 1-0 na Wazalendo wiki iliyopita. Strathmore ya kocha, Meshack Senge ilitangulia kupata bao la kwanza kupitia Seth Onyango kabla ya Douglas Nyerere kusawazishia Sailors.

Kisha iliongeza bao la pili lililofumwa na Alfa Musambi. Nao Victor Omwenda na Ibrahim Mose kila mmoja alifungia Sailors bao moja na kuisadia kubeba alama zote tatu.

”Nashukuru wenzangu kwa kazi nzuri waliofanya kwenye mchezo huo na kutwaa ufanisi wa pointi zote,” nahodha wa Sailors Moses Omama alisema.

Kwenye kampeni za Supa Ligi ya wanaume, Parkroad Badgers iliandikisha ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) kwenye mechi iliyopigiwa uwanjani humo.

Parkroad Badgers ilivuna ufanisi huo kutokana na mabao ya Andrew Kamau, John Kaloki, Gordon Oduor na Evanson Alulu walitikisha wavu mara moja kila mmoja. Nayo KU ilijipatia bao la kufuta machozi kupitia Daniel Mwangi.

Kwenye ligi ya taifa kwa wanaume, Thika Rovers ilihimili makali ya wapinzani wao na kusajili ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wazalendo Youth.