Suala la ardhi latumiwa kama chombo kumega kura za Pwani

Suala la ardhi latumiwa kama chombo kumega kura za Pwani

Na PHILIP MUYANGA

Ni donda ndugu ambalo kila wakati wa siasa unapofika kama ilivyo sasa kinatoneshwa na wale wanaojitakia nyadhifya mbalimbali hususan zile za urais.

Kidonda chenyewe ni swala la ardhi ambalo limesumbua maeneo mengi ya Pwani kwa muda mrefu bila suluhu yoyote kupatikana.Kila wakati wa siasa unapowadia,utawasikia wanasiasa wakilivalia njuga swala la ardhi huku Pwani huku wakitoa ahadi chungu nzima ya kuwa watalitatua.

Kwa miaka mingi wanasiasa wengi wanaotaka urais na wale wanotaka viti mbali mbali katika eneo la pwani wanapenda kusisimua hisia za wapiga kura kupitia swala la ardhi, ambao kwao limekuwa ni chambo kikuu cha kuwavutia wapigakura.

Hivi maajuzi katika ziara zake la Azimio la Umoja huku Pwani, kinara wa chama cha Orange Democratic Movement Raila Odinga aliahidi kuliangalia suala la ardhi na kuhakikisha suluhu ya mizozo ya ardhi imepatikana.

TATUA

Na miezi michache serikali ya Jubilee iliposhika uongozi mwaka wa 2013, naibu Rais William Ruto alisema watatatua swala la ardhi Pwani akisema kuwa limekuwa likitumiwa kama chombo cha kampeni.Miaka zaidi ya tisa baadaye tangu serikali ya Jubilee kutwaa uongozi,haijatatua swala la ardhi licha ya kutoa hati miliki kwa wakaazi wachache na kununua shamba la Waitiki.

Swala la wanasiasa kufanya ardhi kama chambo cha wao kupigiwa kura limeonekana kuwakera wananchi wengi hususan maskwota ambaao wanaamini kuwa limekuwa likitumiwa kisiasa kwa manufaa ya wanaotaka uongozi.Wachanganuzi wa siasa wamekubaliana ya kuwa swala la ardhi ni jambo ambalo linazua mihemko ya hisia za watu wengi ndiposa wanasiasa wengi wanapenda kulitumia kama kigezo cha kampeni zao.

Prof Halimu Shauri ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Pwani anasema kuwa swala la ardhi linatumiwa na wanasiasa ambao hawana ajenda yeyote kwa wapiga kura.Anasema wanasiasa hao huongea kuhusu ardhi kwa kuwa wana hamu ya mamlaka na sio ati wanapenda kutatua swala hilo.

“Jambo la ardhi ni la zamani kwa kuwa hakuna mwelekeo mwafaka wa kulitatua,” alisema Prof Shauri.Aliilimbikizia lawama pia tume huru ya uchaguzi na mipaka nchni (IEBC) kwa kukosa kutoa maelimisho ya upigaji kura kwa wananchi ili wachague viongozi wanaowafaa.

“IEBC inafaa kuendeleza maelimisho ya upigaji kura kwa miaka mitano mfululizo na sio kugoja hadi wakati kura unapofika,” alisema Prof Shauri.Prof Shauri alisema kuwa swala la upeanaji wa hati miliki kwa baadhi ya wakazi ni kama zawadi ambayo haitatui hali halisi ya swala la ardhi.

Kwa upande wake wakili Shukran Mwabonje alisema kuwa wanasiasa hutumia swala la ardhi kwa kuwa wanajua linavuta hisia kali kwa wapiga kura.“Wanasiasa wanatumia swala hili la ardhi ili kujipatia nafasi katika siasa na kujaribu kushinda viti vya kisiasa,” alisema Bw Mwabonje.

PENDEKEZO

Bw Mwabonje aliongeza kusema kuwa mwaka wa 2015, tume ya kitaifa ya kusimamia maswala ya ardhi (NLC) ilitoa pendekezo kwa bunge la kitaifa kuhusiana mswaada ambao utatatua dhuluma za hapo awali za mambo ya ardhi kwa mara moja.

Bw Mwabonje alisema kuwa mswaada huo The Investigation & Adjudication of Historic Land Injustice Bill, 2015 haujawahi kupitishwa hadi leo.Mchanganuzi wa maswala ya kisisa Bi Maimuna Mwidau naye aliunga mkono hoja ya kuwa swala la ardhi linatoa hisia kali kwa wananchi ndiposa wanasiasa wanalitumia.

Bi Mwidau aliongeza kusema kuwa swala la ardhi ni njia moja ya wanasiasa wanatumia kutafuta umaarufu na uungwaji mkono.Mchanganuzi huyo wa siasa alisema kuwa baadhi ya mabwenyenye, watu wenye ushawishi na hata wafanyibiashara wamechukua ardhi za umma na inakuwa vigumu swala hilo kutatuliwa ndiposa linatumiwa kama kigezo katika kampeni.

“Baadhi ya wabunge wanaochaguliwa hawaliangazii swala hili bungeni ipasavyo wanalitumia tu kisiasa, swala hili lingekuwa limetatuliwa,” alisema Bi Mwidau.Bi Mwidau aliongeza kusema kuwa wapiga kura wengi ni maskini na kwamba haja yao ni chakula na hawana nafasi ya kuwauliza wanasiasa maswali.

Naye wakili Yusuf Aboubakar alisema kuwa tatizo la ardhi ni mipango bora kwani hata kama kuna ramani za ardhi mipango hiyo haifuatiliwi.Alisema kuwa mipango bora, huhusisha wananchi katika upangaji wa maswala ya ardhi na kuondoa ufisadi katika afisi za sajili za ardhi ndio kunaweza kuwa suluhu ya mambo ya ardhi katika eneo la pwani.

Ingawa swala la ardhi ndilo kidonda kikuu kinachosumbua wapwani, pia swala la mbuga za wanyama za Tsavo limetumiwa sana na baadhi ya wanasiasa katika kampeni zao.Wengi wa wanasiasa huwaahidi wapiga kura kuwa iwapo watachaguliwa basi watahakikisha mapato yote ya mbuga hizo yatarudi katika kaunti ya Taita Taveta, tofauti na ilivyo sasa mapato hayo yanaenda kwa serikali kuu.

“Tumezoea kudangaywa kila wakati na jambo hili la Tsavo, wanalitumia kisiasa na hawana nia yoyote ya kulitatua,”alisema mkaazi mmoja wa Voi aliyetaka jina lake libanwe.Kwa kipindi hiki cha siasa wakazi wengi wa pwani watarajie wanasiasa wao wapige kampeni kwa wingi huku wakitumia swala la ardhi au la mbuga za wanyama za Tsavo kama vigezo vya kampeni zao za kusaka viti mbalimbali vya uongozi kitaifa, bungeni,kaunti na hata maeneo ya uwakilishaji wa wadi.

You can share this post!

Zaidi ya Sh1.5M zachangiwa Congo Boys FC

JAMVI: Safari ya OKA, MKF imejaa visiki vingi

T L