Michezo

Suarez awakejeli wenzake kuaibishwa na Liverpool

May 8th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa Barcelona Luis Suarez amewakashifu wachezaji wenzake baada ya kulishwa kichapo kizito cha 4-0 na Liverpool katika nusu fainali ya Klabu Bingwa Barani Uropa Jumanne Mei 7 ugani Anfield.

Barcelona waliingia kwenye mechi hiyo wakiwa kifua mbele 3-0 ila wakaaibishwa kwa jumla ya mabao 4-3 kwenye mechi ya mkondo wa pili.

Akizungumza baada ya mechi, Suarez alisema wenzake walishindwa kukabili Liverpool ilhali mchuano huo ulikuwa wenye umuhimu mkubwa kwao.

“Tumesikitika na tumeathirika kabisa kisaikolojia. Ni wakati wa kila mchezaji kujihoji na kujiangalia iwapo anafaa kulaumiwa kwa matokeo hayo. Hatuwezi kutenda kosa sawa miaka miwili ikifuatana na lazima tufikirie na kuambiana ukweli kuhusu mambo tuliyoyafanya visivyo,” akasema Suarez.

“Si kawaida kwamba katika muda wa dakika moja tunafungwa mabao mawili. Tulizidiwa ni kana kwamba tulikuwa timu ya vijana,”akaongeza Suarez.

Suarez alifungua ukurasa wa mabao kwa Barcelona juma moja lililopita ugani Camp Nou lakini hakuweza kupata bao dhidi ya timu yake ya zamani Liverpool.

Barcelona ambao walipitia hali kama hiyo msimu wa 2017/2018 mikononi mwa As Roma ya Italia sasa watasubiri hadi msimu wa 2019/20 kuwania kushinda taji hilo.