Michezo

Suarez, Messi na Umtiti wapona

June 12th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

VIGOGO Luis Suarez na Lionel Messi wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona kitakachovaana na Real Mallorca usiku wa Juni 13, 2020 katika kipute cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kilichorejelewa Juni 11 kwa gozi kati ya Sevilla na Real Betis.

Likizo ya lazima iliyochangiwa na janga la corona katika soka ya Uhispania ilimpa Suarez, 33, fursa ya kupona jeraha la goti la kulia lililohitaji upasuaji mnamo Januari 2020.

Messi ambaye anaongoza orodha ya wafungaji bora wa La Liga alikuwa na jeraha la paja. Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 32 alirejea mazoezi wiki hii na kupiga jeki kikosi cha Barcelona kinachojiandaa kwa mchuano wa kwanza baada ya siku 97 mapumzikoni.

“Messi na Suarez wako katika hali shwari na watakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Mwanzo, Suarez yuko katika hali nzuri zaidi kuliko jinsi tulivyotarajia. Tatizo la pekee huenda ni ubora wa fomu hasa ikizingatiwa kwamba amekuwa nje kwa kipindi kirefu zaidi,” akasema kocha Quique Setien.

Beki Samuel Umtiti anayemezewa na Arsenal pia yuko katika hali nzuri ya kuwajibishwa. Difenda chipukizi mzawa wa Uruguay, Ronald Araujo, 21, anatarajiwa kuwa kizibo cha Clement Lenglet wa Ufaransa ambaye anatumikia marufuku ya mechi tatu.

Real Madrid waliwapita Barcelona kileleni mwa jedwali la La Liga mnamo Machi 1 baada ya kuwapokeza kichapo cha 2-0 uwanjani Santiago Bernabeu.

Hata hivyo, Barcelona walirejea kileleni mnamo Machi 7 baada ya penalti ya Messi aliyefunga bao lake la 19 kufikia sasa msimu huu, kuwapa mabingwa hao watetezi ushindi wa 1-0 dhidi ya Real Sociedad uwanjani Nou Camp nao Real wakapepetwa 2-1 na Real Betis siku iliyofuata.

Zikisalia mechi 11 zaidi, Barcelona wanajivunia alama 58, mbili zaidi kuliko Real watakaovaana na Eibar mnamo Juni 14, 2020. Mallorca ambao watakuwa wenyeji wa Barcelona mnamo Juni 13 wananing’inia padogo mkiani mwa jedwali licha ya kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Eibar katika mechi yao ya mwisho.